TUC: Nusu ya wanawake Uingereza wananyanyaswa kingono makazini
Uchunguzi uliofanywa na shirika moja linalojulikana kwa jina la Trades Union Congress TUC kwa kifupi unaonesha kuwa, nusu ya wanawake nchini Uingereza wamekuwa wakinyanyaswa kingono katika maeneo yao ya kazi.
Uchunguzi huo unaeleza kuwa, wanawake hao wamekuwa wakitumiwa vibaya kingono katika maeneo yao ya kazi na kufanyiwa utani usiofaa. Uchunguzi huo, huo uliotolewa leo unaonyesha kwamba, asilimia 80 ya wanawake hao wanaofanyiwa unyanyasaji huo wa kingono hushindwa kuripoti kwa waajiri wao kwa kuhofia kuharibika uhusiano wao katika mazingira ya kazini.
Alice Hood, mmoja wa maafisa wa shirika la Trades Union Congress TUC nchini Uingereza amesema kuwa, visa vingi vya wanawake kunyanyaswa kingono nchini humo ni jambo la kushtusha mno na kuna haja ya jambo hilo kuchukuliwa kuwa ni kengele ya hatari.
Ameongeza kuwa, unyanyasaji wa kingono wanaofanyiwa wanawake katika maeneo ya kazi lingali moja ya matatizo makubwa yanayowakabili wanawake nchini Uingereza na tatizo hilo halijakwisha.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, takribani mwanamke mmoja kati ya watano amenyanyaswa kingono na mkubwa wake wa kazi nchini Uingereza na wanawake hao wamekuwa hawashtaki kutokana na kuona kuwa, hakuna atakayefuatilia suala lao.
Wachunguzi wa shirika la TUC wanasema kuwa, hali ya unyanyasaji wa kingono makazini kwa wanawawake wenye umri kati ya miaka 16 hadi 24 ni mbaya zaidi nchini humo ikilinganishwa na wanawake wengine ambapo theluthi mbili ya wanawake hao wametangaza kuwa, wamewahi kunyanyaswa kingono katika maeneo yao ya kazi.
Frances O'Grady, Katibu Mkuu wa Trades Union Congress ametangaza kuwa, tatizo hilo limekuwa likiwafanya wanawake hao kukabiliwa na matatizo ya kiroho na kuhisi kudhalilishwa na huenda hali hiyo ikapelekea kukumbwa na madhara makubwa ya kisaikolojia.