Vifo vya wanaotumia madawa ya kulevya Uingereza vyavunja rekodi
Takwimu mpya na rasmi zilizotolewa nchini Uingereza zinaonyesha kuwa, idadi ya watu wanaopoteza maisha nchini humo kutokana na kutumia madawa ya kulevya imeongezeka mno na haijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo ya bara Ulaya.
Takwimu hizo zimepokelewa kwa hisia mseto nchini Uingereza na hata kupelekea kukosolewa vikali sera za serikali ya London katika uwanja huo.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza imetangaza kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha nchini humo mwaka jana kutokana na kutumia madawa haramu ya kulevya na yale yaliyoruhusiwa kisheria ilifikia 3,647. Hii ni katika hali ambayo, mwaka wa kabla yake yaani 2014 idadi hiyo ilikuwa 3,346.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo idadi ya watu wanaoaga dunia nchini uingereza kutokana na kutumia madawa ya kulevya ya heroini na kokeini imeongezeka mno nchini humo kuanzia mwaka 1993.
Matokeo ya utafiti mpya yanaonyesha kuwa sehemu za kazi za wafanyakazi wa Uingereza zaidi ya milioni moja zina madawa ya kulevya. Gazeti la Daily Mail liliwahi kuripoti kuwa ripoti zilizochapishwa na polisi ya London zinaeleza kuwa wafanyakazi wa Uingereza hutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa mwaka kwa ajili ya kununulia madawa ya kulevya. Baadhi ya watu hao wanafanya kazi kama zile za upasuaji, ualimu na udereva huko Uingereza.
Ofisi ya kupambana na madawa ya kulevya na jinai ya Umoja wa Mataifa iliwahi kutangaza kuwa, Uingereza imebadilika na kuwa soko kuu la madawa ya kulevya aina ya kokeini kati ya nchi za Ulaya.
Hivi sasa serikali ya Waziri Mkuu Theresa May inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia kuongezeka vifo vya watu wanaotumia madawa ya kulevya nchini Uingereza.