Chama cha Liberal Democrats chataka kura mpya ya maoni kuhusu Brexit
Chama cha Liberal Democrats nchini Uingereza kimetoa wito wa kuitishwa kura mpya ya maoni kuhusu uamuzi wa nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.
Chama hicho kimetangaza kuwa, kitapiga kura ya kupinga suala la kuanza mazungumzo ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya katika Bunge la nchi hiyo ila kama serikali itaahidi kuitisha kura mpya ya maoni juu ya kujiondoa katika umoja huo.
Kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, Tim Farron amesema, chama chake kitapiga kura ya kupinga zoezi la kuanza mazungumzo ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mpaka pale serikali ya London itakaporuhusu kuitishwa kura mpya ya maoni juu ya suala hilo.
Chama hicho kina viti vichache katika Bunge la Uingereza lakini wito huo unapata nguvu zaidi kwa kutilia maanani kwamba, baadhi wa wabunge wa chama cha upinzani cha Leba pia wameapa kupiga kura dhidi ya kuanza zoezi la mazungumzo ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, Waingereza wengi wanajuta kupiga kura ya kujiondoa nchi yao katika Umoja wa Ulaya.