Jeshi la Myanmar laua makumi ya Waislamu wa Rohingya
Jeshi la Myanmar limeua makumi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika wimbi jipya la ukandamizaji unaofanyika nchini humo dhidi ya jamii hiyo ya waliowachache hususan katika mkoa wa Rakhine.
Mauaji ya Waislamu hao yanatajwa kuwa ni ya aina yake tangu baada ya kuanza wimbi jipya la machafuko katika jimbo hilo la kaskazini magharibi mwa Myanmar.
Utawala wa Myanmar umefunga kabisa njia zote za kuelekea katika eneo hilo na kutatiza suala la kupata habari zaidi na kuhusu ukweli wa madai yanayotolewa na jeshi la nchi hilo ambalo limesema kuwa Waislamu hao ni wanachama wa kundi la waasi.
Wanadiplomasia wa nchi za kigeni nchini Myanmar wanasema, mauaji ya idadi hiyo kubwa ya Waislamu wa Rohingya yanaondoa matumaini ya kutatuliwa haraka mgogoro huo wa kihistoria na kutekelezwa marekebisho ya kijamii katika eneo hilo.
Jimbo la Rakhine lina zaidi ya Waislamu milioni moja na maelfu miongoni mwao wameuawa na malaki ya wengine kulazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.
Siku chache zilizopita mamia ya nyumba za Waislamu wa Myanmar zilichomwa moto magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kuendelea ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch jana Jumapili lilionesha picha za satalaiti zinazoonyesha nyumba za Waislamu wa Rohingya magharibi mwa Myanmar zikichomwa moto. Afisa mmoja wa shirika hilo kanda yha Asia amesema kuwa, uharibu uliofanywa dhidi ya nyumba za Waislamu hao ni mkubwa kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.