Trump: Marekani inapaswa kuwa mbele katika uwanja wa silaha za nyuklia
(last modified Fri, 24 Feb 2017 04:51:24 GMT )
Feb 24, 2017 04:51 UTC
  • Trump: Marekani inapaswa kuwa mbele katika uwanja wa silaha za nyuklia

Rais Donald Trump wa Marekani ametoa matamshi yanayogongana akitoa wito wa kuzuiwa uenezaji wa silaha za nyuklia na wakati huo huo akisisitiza kuwa, Washington daima inapaswa kuwa na maghala makubwa zaidi ya silaha za nyuklia kuliko nchi nyingine zote duniani.

Rais wa Marekani ambaye amedai kuwa nchi yake inataka kuwepo dunia isiyo na silaha za nyuklia amesema kuwa, pamoja na hayo Marekani kamwe haitabakia nyuma ya hata nchi marafiki katika uwanja wa kumiliki silaha za atomiki. 

Donald Trump ameyataja makubaliano ya miaka 10 kati ya Marekani na Russia yanayojulikana kwa jina la New Start ambayo yanazipa fursa pande hizo mbili kupunguza silaha za nyuklia hadi kufikia mwaka ujao wa 2018 kwamba ni makubaliano ya upande mmoja. Ameyalinganisha makubaliano hayo na yale ya nyuklia ya Iran (JCPOA) na kusema, haya pia ni makubaliano mengine mabaya yaliyowahi kufanywa na Marekani.

Donald Trump

Rais Donald Trump wa Marekani pia ameashiria majaribio ya silaha za nyuklia yaliyofanywa na Korea Kaskazini na kusema kuwa, yameikasirisha sana serikali ya Washington.

Ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na Taasisi ya Amani na Stockholm inakadiria kuwa, mwanzoni mwa mwaka wa 2016 Marekani ilikuwa na makombora elfu 7 ya atomiki.