Marekani, Korea 2 na Japan ziko katika ncha ya kupigana
Washington imeanza kutuma nchini Korea Kusini mfumo wa ulinzi wa makombora wa THAAD, baada ya Korea Kaskazini kusema kuwa, jaribio lake la hivi punde la makombora ni maandalizi kwa ajili ya kuzishambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Japan.
Katika mazungumzo ya simu, Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wamesema majaribio haya mapya ya makombora yaliyofanywa na Korea Kaskazini ni vitisho vilivyoingia katika 'hatua mpya'.
Abe amesema chokochoko hizo za Korea Kaskazini zinakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni changamoto sio tu kwa eneo, bali kwa jamii ya kimataifa.
Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA limeripoti kuwa, Rais wa nchi hiyo Kim Jong-un binafsi ndiye aliyeagiza na kufuatilia kwa karibu kufanyiwa majaribio makombora hayo kwa kile alichokitaja kuwa, kujiandaa kukabiliana na mababeru.
Hapo jana, Pyongyang ilifanyia majaribio makombora manne, ambapo matatu yalidondoka nchini Japan kwa mujibu wa serikali ya Tokyo.
Hapo jana Baraza la Usalama la UN lilitangaza kuwa litafanya kikao kesho Jumatano kujadili kadhia hiyo ya Korea Kaskazini. Kadhalika Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekosoa majaribio hayo mapya ya makombora ya Korea Kaskazini na kuitaka nchi hiyo ijiepusha na 'uchokozi zaidi'.