Trump awashambulia marafiki na maadui zake
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48732-trump_awashambulia_marafiki_na_maadui_zake
Tangu aingie madarakani nchini Marekani mwezi Januari 2017, Rais Donald Trump wa nchi hiyo amekuwa akitekeleza siasa ambazo zimeifanya dunia kuwa uwanja wa malumbano na mivutano.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 12, 2018 02:41 UTC
  • Trump awashambulia marafiki na maadui zake

Tangu aingie madarakani nchini Marekani mwezi Januari 2017, Rais Donald Trump wa nchi hiyo amekuwa akitekeleza siasa ambazo zimeifanya dunia kuwa uwanja wa malumbano na mivutano.

Rais huyo aliye na majivuno mengi amekuwa akiwashambulia marafiki na maadui wake bila kujali na ndio maana uhusiano wa nchi hiyo na nchi nyingi za Asia Mashariki na za pande mbili za Bahari ya Atlantic umeingia dosari kubwa. Wakati huohuo uamuzi wa rais huyo wa kuiondoa nchi yake katika mikataba muhimu ya kimataifa umezusha mivutano mikubwa ya kieneo na kimataifa. Kwa kufuatilia sera za upande mmoja na za kidikteta, Trump anataka kuzitwisha nchi nyingine mitazamo na matakwa yake, yakiwemo matakwa ya kibiashara. Marie-Cécile Naves mtafiti wa Ufaransa anasema kuwa siasa za Trump ni siasa za mabavu, vitisho na za maslahi ya  kibinafsi. Akizugumza hivi karibuni katika mkusanyiko wa kampeni za uchaguzi mdogo nchini Marekani, Trump kwa mara nyingine aliashiria siasa zake za nje ambapo alikosoa na kuwakejeli waziwazi maarafiki na maadui wake. Alikariri misimamo yake kuhusiana na Umoja wa Ulaya, Nato, Ujerumani, China, Japan, Korea Kusini, Korea Kaskazini, Saudi Arabia na Iran na kudai kuwa kutokana na misimamo yake hiyo Marekani imeanza tena kuheshimiwa duniani.

Trump akiwa na watawala wa nchi za Kiarabu

Huku akikosoa siasa za nchi za Ulaya za kulinda maslahi ya viwanda vyao, Trump alisema: "Hata kama kidhahiri Umoja wa Ulaya unaonekana kuwa mzuri na wa kuvutia lakini hauna huruma na umebuniwa kwa ajili ya kunufaika na sisi."

Kwa mara nyingine Tump aliishambulia kwa maneno makali China kwa kusema kuwa kwa miaka mingi sasa nchi hiyo ya Asia imekuwa ikipata faida kubwa ya mabilioni ya dola kutoka kwa Wamarekani, lakini kwamba baada ya yeye kuingia madarakani mwenendo huo utakomeshwa. Trump pia alizishambulia kwa maneno makali nchi za Japan na Korea Kusini na kudai kwamba licha ya kuwa Marekani inalipa gharama kubwa kwa ajili ya kuzilinda nchi hizo lakini Japan inaitumia vibaya Marekani. Rais huyo wa Marekani alikariri tena udharura wa nchi hiyo kulipwa na Saudi Arabia kutokana na ulinzi inaopewa nchi hiyo ya Kiarabu. Akiashiria uamuzi wake wa kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA, Trump alitetea aumuzi huo kwa kusema: "Kabla zijakuwa rais wa Marekani, Iran ingeweza kuvamia na kulidhibiti eneo zima la Mashariki ya Kati katika kipindi cha dakika 12." Wakati huohuo amedai kwamba hivi sasa Marekani inaunda jeshi lenye nguvu kubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa duniani.

Trump akijitoa katika moja ya mapatano muhimu ya kimataifa

Matamshi ya rais huyu mbabe yanabainisha wazi kwamba anaiona dunia ikiwa mdaiwa wa Marekani. Kwa mtazamo wake, sehemu moja ya dunia ambayo inaundwa na nchi kama vile China na Ulaya inaitumia vibaya Marekani na sehemu nyingine yaani washirika wa kieneo wa Washington kama Japan, Korea Kusini na Saudi Arabia inabebwa bure na Marekani.

Katika upande wa pili, kwa kueneza propaganda na madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran, Trump anajarifu kuzua hofu wa wasiwasi duniani dhidi ya serikali ya Tehran. Kupitia nara yake ya 'Marekani Kwanza' Trump anajaribu kuyapa kipaumbele maslahi ya Marekani kwa madhara ya mataifa mengine duniani akidhani kwamba jambo hilo litaipa nchi yake nguvu zaidi katika upeo wa kimataifa na hivyo kumuwezesha kuwashinda washindani wake. Pamoja na hayo tathmini ya siasa za upande mmoja za mtawala huyo mbabe inabainisha wazi kwamba hazijakuwa na natija yoyote ghairi ya kuifanya Marekani iendelee kutengwa duniani.