Bunge la Australia lamjia juu Seneta mwenye chuki dhidi ya Waislamu
(last modified Thu, 04 Apr 2019 02:35:07 GMT )
Apr 04, 2019 02:35 UTC
  • Bunge la Australia lamjia juu Seneta mwenye chuki dhidi ya Waislamu

Bunge la Australia limepiga kura kwa kishindo kupasisha hoja ya kumlaani na kumkosoa Seneta mwenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia, kutokana na matamshi yake ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu baada ya shambulizi la kigaidi la mwezi uliopita nchini New Zealand.

Maseneta hao wamepasisha kwa kauli moja hoja hiyo ya kumkosoa Seneta Fraser Anning, wakisisitiza kuwa matamshi yake ya kuwalaumu wahanga wa shambulizi hilo la kigaidi nchini New Zealand hayaashirii msimamo wa Seneti wala wananchi wa Australia.

Seneta Manning alidai kuwa, shambulio hilo la kigaidi lilisababishwa na kuendelea kuongezeka kwa kasi kubwa idadi ya Waislamu na wahajiri sio tu New Zealand pekee, bali katika nchi za Magharibi kwa ujumla.

Seneta Mathias Cormann wa Chama cha Kiliberali alisema katika kikao cha jana Jumatano, "Matamshi ya Seneta Anning yalikuwa ya kukera na kusikitisha. Ni jambo zuri namna maseneta wameungana na kwa kauli moja wameipigia kura hoja ya kukosoa kauli hiyo."

Itakumbukwa kuwa, watu wasiopungua 50 wakiwemo wanawake na watoto wadogo waliuawa na wengine wengi wakijeruhiwa katika mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini New Zealand wakati waumini wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya Ijumaa mnamo Machi 15.

Gaidi mwenye chuki dhidi ya Uislamu aliyehusika katika hujuma ya kigaidi ya New Zealand alitangaza kuwa mfuasi wa Trump

Hii sio mara ya kwanza kwa maseneta wa Australia kuonyesha wazi wazi chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo. Mwaka 2017, Seneta Pauline Hanson, ambaye ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha One Nation aliingia Bungeni akiwa amevalia burqa huku maseneta wa chama chake wakicheka kwa dharau.

Seneta huyo alifanya hivyo akiwa na lengo la kulikejeli na kulivunjia heshima vazi hilo linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu.