Uturuki: Ufaransa na Israel zilitaka kuunda 'dola la kigaidi' Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zilikuwa na hamu kubwa ya kuunda dola la kigaidi ndani ya ardhi ya Syria.
Mevlüt Çavuşoğlu alisema hayo jana Ijumaa na kusisitiza kuwa, "Walitaka kuunda dola la kigaidi huko (Syria) na njama hizi ziliongozwa na Ufaransa na Israel."
Ufaransa imesitisha mauzo ya silaha zake kwa Uturuki kutokana na operesheni ya kijeshi ya Ankara kaskazini mwa Syria huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukisema kuwa unatathmni uwezekano wa kuwapa silaha wapiganaji wa Kikurdi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameituhumu serikali ya Ufaransa kuwa inayaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi huko Syria haswa kundi la PKK na tawi lake la wanamgambo wa YPG.
Jumatano iliyopita, Bunge la Ufaransa lilipasisha azimio la kuwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi, ambao Uturuki imekuwa ikiwalenga katika operesheni yake ya Chemichemi ya Amani huko kaskazini mwa Syria.
Siku ya Alkhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilimuita balozi wa Ufaransa nchini humo kulalamikia azimio hilo, na kisha kutoa taarifa iliyosema, "Ni wazi wamefikia uamuzi huu baada ya mpango wao wa kuunda dola la kigaidi ndani ya Syria kugonga mwamba."