Ukosoaji wa Pakistan dhidi ya serikali ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57111-ukosoaji_wa_pakistan_dhidi_ya_serikali_ya_marekani
Pakistan imeyakosoa vikali madai ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kwamba, Islamabad haina uwezo wa kupambana na ugaidi na kuyataja matamshi hayo kuwa siyo ya kukubalika hata kidogo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 07, 2019 03:29 UTC
  • Ukosoaji wa Pakistan dhidi ya serikali ya Marekani

Pakistan imeyakosoa vikali madai ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kwamba, Islamabad haina uwezo wa kupambana na ugaidi na kuyataja matamshi hayo kuwa siyo ya kukubalika hata kidogo.

Muhammad Faisal, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan amesema kuwa, licha ya kuwa, mataifa ya dunia yanakiri kwamba, Islamabad inapambana na ugaidi, lakini Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imekana katika ripoti yake ya hivi karibuni nafasi athirifu ya Pakistan katika kupambana na ugaidi katika eneo.

Muhammad Faisal amekosoa vikali ripoti ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani na kusema kuwa, inakinzana na matamshi ya baadhi ya viongozi wa nchi hiyo yanayosisitiza mchango na nafasi muhimu na athirifu ya Pakistan katika kurejesha amani na uthabiti katika eneo. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan amesisitiza pia kuwa, Islamabad imethibitisha nia yake njema kuhusiana na suala la kurejesha amani na uthabiti katika eneo kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la mchakato wa amani huko nchini Afghanistan.

Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan katika mazungumzo yake na  Rais Donald Trump wa Marekani

Hatua ya Marekani ya kuituhumu Pakistan kwamba, ina undumakuwili katika kukabiliana na ugaidi, ni utendaji ambao ulianza kutekelezwa na Washington tangu mwaka 2004 na hivyo kupelekea kutanda wingu zito katika uhusiano wa nchi mbili hizo. Katika kipindi cha zaidi ya miaka 11 iliyopita, uhusiano wa Marekani na Pakistan umegubikwa na tuhuma za Washington dhidi ya Islamabad kwamba, inaliunga mkono kundi la wanamgambo wa Taliban na hata kushirikiana nalo. Mwenendo huo umeufanyya uhusiano kati ya Washington na Islamabad ugubikwe na hali ya mzozo na mvutano.

Serikali ya Marekani inadai kwamba, Pakistan imeanzisha mchezo mchafu na wa kindumakuwili katika kupambana na ugaidi; kwani sambamba na kusisitiza ulazima wa kukabiliana na ugaidi ambao kwa sasa ni tishio la ulimwengu mzima, imekuwa pia ikiyaunga mkono baadhi ya makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na hivyo kuhatarisha mipango ya Marekani na washirika wake huko Afghanistan na hata katika uga wa kieneo.

Muhammad Yusuf Zazi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kijeshi wa Afghanistan anasema: Kuna mapango na kambi za magaidi katika miji ya Pakistan, na mashirika ya kiusalama na kiinteliijensia ya nchi hiyo yana taarifa kamili na za kina kuhusiana na jambo hilo.

Wanamgambo wa Taliban

Matamshi ya Rais Donald Trump Agosti 2017 ilikuwa nukta ya kuanzia ya kutumia lugha za kejeli na kali dhidi ya Pakistan, matamshi ambayo yalichochea na kushadidisha mzozo na hitilafu baina ya nchi mbili hizo. Hatua ya Trump ya kusema kuwa, Pakistan imo mbioni kubadilika na kuwa kimbilio na maficho salama ya magaidi yalifuatiiwa na nchi hiyo kuikatia misaada Islamabad.

Fauka ya hayo, tuhuma za Trump dhidi ya viongozi wa Pakistan kwamba, walifanya hadaa kwa ajili ya kupokea mabilioni ya dola kutoka White House katika kipindi cha uongozi wa Marais George W. Bush na Barack Obama ziliwakasirisha mno wananchi wa Pakistan na viongozi wa nchi hiyo.

Licha ya kuwa, msimu wa joto uliopita, Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan alifanya safari huko Washington ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump, lakini safari yake hiyo pamoja na mazungumzo yake havikusaidia kupunguza kiwango cha mvutano katika uhusiano wa nchi mbili hizo.

Hasa kwa kutilia maanani kwamba, wakati Imran Khan alipokuwa mpinzani alikuwa katika kundi la wapinzani wa siasa za Marekani na mara chungu nzima aliongoza maandamano dhidi ya serikali ya Washington.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan 

Kwa kuzingatia misimamo hiyo ya Imran Khan alipokuwa mpinzani, kuna dhana hii kwamba, Waziri Mkuu huyo hayuko tayari kulegeza misimamo yake mkabala na siasa za kibeberu za Marekani. Katika mazingira kama haya, kuna uwezekkano wa walimwengu kuendelea kushuhudia mizozo na mivutano kati ya Marekani na Pakistan.

Serikali ya Marekani sanjari na kuituhumu Pakistan kwamba, inaamiliana kindumakkuwili na ugaidi, inaituhumu pia nchi hiyo kwamba, imekuwa ikikwamisha mchakato wa amani nchini Afghanistan, msimamo ambao unasisitizwa na kutiliwa mkazo pia na serikali ya Kabul.

Hata hivyo inapasa kuzingatiwa kwamba, ndani ya Marekani kwenyewe hakuna msimamo mmoja kuhusiana na nafasi ya Pakistan katika kupambana na ugaidi, kwani baadhi ya shakhsia serikalini na katika Kongresi ya nchi hiyo hawapingi na kukanusha nafasi ya Islamabad katika kupambana na misimamo ya kufurutu ada.