EU yatofautiana na US kuhusu uporaji wa ardhi za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57361-eu_yatofautiana_na_us_kuhusu_uporaji_wa_ardhi_za_wapalestina
Umoja wa Ulaya umeshikilia msimamo wake kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni haramu na kinyume cha sheria za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2019 04:36 UTC
  • EU yatofautiana na US kuhusu uporaji wa ardhi za Wapalestina

Umoja wa Ulaya umeshikilia msimamo wake kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni haramu na kinyume cha sheria za kimataifa.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini amesema katika taarifa kuwa, "Msimamo wa Umoja wa Ulaya juu ya sera ya Israel kuhusu upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu upo pale pale na wala haujabadilika."

Ameutaka utawala haramu wa Israel ukomeshe mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wake katika maeneo ya Palestina unayoyakalia kwa mabavu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Matamshi ya afisa huyo wa ngazi za juu wa EU yanaonekana kuwa radimali kwa kauli ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyetangaza kuwa Marekani imeangalia upya suala hilo la ujenzi wa nyumba za Wazayuni maghasibu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Netanyahu akizindua ujenzi wa vitongoji vipya ya Wazayuni kwa heshima ya Trump

Pompeo amesema utawala wa Marekani hautambui tena uporaji wa ardhi na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Hatua ya Marekani ya kuangalia upya sera yake hiyo ya tangu mwaka 1978 inaenda kinyume kabisa na kukanyaga msimamo wa taasisi za kimataifa kama EU, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na hata Wapalestina wenyewe.