Trump: FBI ilitaka kupindua serikali yangu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57470-trump_fbi_ilitaka_kupindua_serikali_yangu
Rais Donald Trump wa Marekani amekosoa vikali mwenendo wa uchunguzi kuhusu kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na kudai kuwa, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilikuwa na nia ya kupindua serikali yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 24, 2019 23:19 UTC
  • Trump: FBI ilitaka kupindua serikali yangu

Rais Donald Trump wa Marekani amekosoa vikali mwenendo wa uchunguzi kuhusu kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na kudai kuwa, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilikuwa na nia ya kupindua serikali yake.

Trump ameyasema hayo huku Kongresi ya nchi hiyo ikichunguza uuwezekano wa kumsaili na kumuuzulu kutokana na kashfa ya Ukrainegate. 

Ripoti iliyotolewa na gazeti la The Guardian la Uingereza imesema kuwa, Trump amekosoa uchunguzi kuhusu faili la kuhusika Russia katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na kusema FBI ilitaka kumpindua kwa kutumia faili hilo.

Donald Trump anadai kuwa mawaziri wa serikali ya rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama wanafanya ujasusi dhidi yake kuhusiana na kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka 2016.

Katika kadhia yya sasa ya Ukrainegate Trump anatuhumiwa kuwa katika mazungumzo yake ya simu na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine hapo tarehe 25 Julai mwaka huu, rais huyo wa Marekani alimtaka  mwenzake huyo wa Ukraine afanye uchunguzi wa ufisadi wa kifedha dhidi ya Joe Biden, mshindani wake mtarajiwa katika uchaguzi wa rais wa mwakani pamoja na Hunter Biden, mtoto wa kiume wa Joe Biden.

Trump anaandamwa na Kongresi katika kashfa ya Ukrainegate

Kufichuliwa mazungumzo hayo kumewafanya Wademocrat katika Bunge la Wawakilishi kuanzisha uchunguzi wenye lengo la kumsaili na kumuuzulu Trump.