Dec 11, 2019 08:11 UTC
  • Mpango wa Pentagon wa kuongeza idadi ya askari wa Marekani barani Ulaya kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa

Donald Trump, rais machachari na mwenye makeke wa Marekani amewahi kusikika mara kadhaa akiwalaumu na kuwakosoa waitifaki wa Washington wa barani Ulaya na hata kutishia kwamba, nchi yake haitakuwa tayari kuendelea kugharimika kwa ajili ya usalama wa nchi za bara hilo; hata hivyo mpango uliotangazwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon wa kuongeza idadi ya askari wa nchi hiyo barani Ulaya umeyatoa maanani madai hayo ya Trump.

Trump

Hatua ya Pentagon ya kutuma askari elfu ishirini wa Marekani barani Ulaya itaweka rekodi ya idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wa Marekani kuweko barani humo katika kipindi cha miaka 25 iliyopita. Maafisa wa jeshi la Marekani wanatangaza kutuma maelfu ya wanajeshi wa nchi hiyo kwa ajili kushiriki mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika nchi za Ulaya, huku uhasama uliopo katika uhusiano wa nchi hiyo na Russia ukizidi kuongezeka. Luteni Jenerali Christopher Cavoli, kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya jeshi la Marekani vilivyoko Ulaya amesema: Askari elfu 20 wa jeshi la Marekani watapelekwa Ulaya mwakani ili kuungana na askari wengine elfu tisa wa nchi hiyo, ambao wengi wao walikuweko barani humo. Kwa mujibu wa Cavoli, lengo la kuchukua hatua za aina hiyo ni "kuonesha uwezo wa kijeshi wa Marekani katika kutuma kwa haraka idadi kubwa ya askari kwa ajili ya kuiunga mkono kijeshi NATO na kutoa jibu kwa mgogoro wowote utakaojitokeza." 

Lakini pia wanajeshi wapatao elfu 37 wa Marekani watashiriki katika mazoezi ya kijeshi yatakayofanyika katika nchi 10 za Ulaya kuanzia mwezi Mei hadi Juni 2020. Kutumwa wanajeshi hao barani Ulaya kutafanyika sambamba na utumaji vifaa na zana elfu 13 za kijeshi barani humo, vikiwemo vifaru, mizinga na magari ya deraya, utakaoanza mwezi Februari mwakani.

Inavyoonesha, licha ya mipango iliyokuwa imepangwa hapo awali ya kupunguza idadi ya askari wa Marekani walioko Ulaya na ambayo ilianza katika kipindi cha urais wa Barack Obama, mabadiliko mapya ya kiusalama yaliyojitokeza barani humo, hasa baada ya kushtadi makabiliano kati ya Russia na shirika la kijeshi la NATO mashariki ya Ulaya kufuatia mgogoro uliozuka nchini Ukraine, yameifanya Washington iangalie upya sera zake za hapo kabla. Kufanyika manuva makubwa katika bara la Ulaya yatakayojulikana kama "Mlinzi wa 2020 Barani Ulaya" (Defender 2020 in Europe) baada ya miaka kadhaa ya mchakato wa kupunguza kuwepo kijeshi Marekani barani humo katika kipindi cha baada ya zama za Vita Baridi (Cold War) kunahesabiwa kuwa nukta muhimu sana katika stratejia ya uga huo. Marekani inadai kuwa, hatua za hujuma za kijeshi zinazofanywa na Russia katika Ulaya Mashariki ni moja ya sababu muhimu za kutekelezwa mkakati huo mpya wa kijeshi. Bila kuashiria kama mlengwa mkuu wa mkakati huo ni Russia, Jenerali Cavoli amesisitiza kuwa: Kuunganishwa eneo la Crimea na Russia kulikofanyika mwaka 2014 kumekuwa sababu ya kutokea mabadiliko katika nyuga zote.

Mkabala na hayo, Russia ina mtazamo ulio kinyume na wa Marekani kuhusu matukio na mabadiliko ya kiusalama yanayojiri barani Ulaya. Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoygu, hatua haribifu za nchi wanachama wa NATO zinazochukuliwa kwa muongozo wa Marekani zimepelekea kuharibika anga ya kiusalama na kuzidi kuvurugika uhusiano wa Moscow na Brussels.

Marekani, ambayo ndiyo iliyoshika hatamu za stratejia za shirika la kijeshi la NATO, kila mwaka inaweka askari na zana zake za kijeshi katika nchi wanachama wa shirika hilo la kijeshi ambazo ni majirani wa Russia, hususan nchi tatu za eneo la Baltiki, yaani Estonia, Latvia na Lithuania. Kwa kufanya hivyo, imekuwa ikizidi kuikaribia mipaka ya magharibi ya Russia, hatua ambayo kwa mtazamo wa Moscow ni tishio kubwa kwa usalama wake wa taifa. NATO, ambayo kutokana na ushawishi wa Marekani ni shirika la kijeshi lenye nguvu, hatua zake zote ambazo imekuwa ikizichukua katika miaka ya karibuni katika uga wa Ulaya zimekuwa zikilenga kukidhi malengo na maslahi ya Washington.

Kuongezeka makabiliano baina ya NATO na Russia mashariki ya Ulaya, kunakoendana na sera za nje za Marekani za kutaka kuidhibiti Russia, kunadhihirisha jinsi shirika hilo la kijeshi linavyotumiwa kiwenzo na kimaslahi na Washington. Muelekeo wa kiuhasama na kiuadui unaofuatwa na NATO kwa kuongeza kwa makusudio maalumu idadi ya askari wake na kufanya mazoezi kadhaa ya kijeshi hususan mashariki ya Ulaya, Bahari ya Baltiki na Bahari Nyeusi, vimeifanya NATO chini ya uongozi wa Marekani, ionekane na Russia kuwa ni tishio kubwa kwa usalama wake wa taifa. Na hii ni hasa baada ya taarifa iliyotolewa wakati wa ufungaji wa kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa NATO kilichofanyika hivi karibuni mjini London, Uingereza, kueleza kinagaubaga kuwa hatua za ushambuliaji za Russia ni tishio kwa usalama wa Ulaya na Amerika ya Kaskazini.../ 

Tags