Janga la corona na indhari ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa kuhusu kudorora uchumi wa dunia
(last modified Sun, 29 Mar 2020 07:49:18 GMT )
Mar 29, 2020 07:49 UTC
  • Janga la corona na indhari ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa kuhusu kudorora uchumi wa dunia

Kuendelea na kuenea mgogoro uliosababishwa na virusi vya corona katika akthari ya nchi duniani kumeibua wasiwasi mkubwa wa kiuchumi kwa kadiri kwamba katika msimamo wake wa hivi karibuni, Bi Kristalina Giorgieva, Mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ameelezea uwezekano wa dunia kuingia katika mdororo wa uchumi kutokana na maambukizo ya virusi hivyo.

Maambukizo ya virusi vya corona duniani yamekuwa na taathira kubwa hasi kwa uchumi wa dunia. Kuenea virusi hivyo katika nchi zote za Ulaya na Marekani kumepelekea kuongezeka wasiwasi kuhusu hali ya uchumi khususan kuwepo uwezekano wa uchumi wa dunia kudorora na taathira zake hasi za kijamii na kisiasa. Huko Ulaya kufungwa vituo vingi vya uzalishaji na viwanda, kupungua ununuzi wa bidhaa, ukosefu wa ajira khususan kusitishwa shughuli za kiuchumi katika nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani humo yaani Ujerumani, ni kengele ya hatari kubwa kwa maafisa wa bara hilo.Taasisi ya Uchumi ya IFO huko Munich imetangaza kuwa uzalishaji wa ndani wa Ujerumani utapungua kuanzia asilimia 5 hadi 20  iwapo corona itaendelea kushuhudiwa nchini humo; na kuwa nchi hiyo inapitia kipindi kigumu zaidi cha kuporomoka kiuchumi baada ya kuungana Ujerumani mbili mwaka 1989. 

Corona nchini Ujerumani na athari zake kwa uchumi wa nchi 

Ili kukabiliana na hali hiyo, viongozi wa nchi za G-20  katika mkutano wao uliofanywa kwa njia ya video wametangaza kuwa watatoa dola bilioni 5000 kwa ajili ya kukabiliana na kuenea maambukizo ya virusi vya corona duniani na kusaidia uchumi wa dunia. Baadhi ya nchi kama Ufaransa zimetangaza kutolewa misaada ya serikali ili kusaidia biashara ndogondogo na kupunguza baadhi ya kodi katika kalibu ya  mpango huo wa pamoja. 

Huko Marekani pia kuporomoka uchumi ni hatari kuu. Baadhi ya makadirio yaliyofanywa nchini humo yanaeleza kuwa mgogoro wa kiuchumi wa mwaka 2008 unaweza kukakariwa huko Marekani iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. Hata imeelezwa kuwa taathira zinazosababishwa na virusi vya corona zinaweza kuisababishia Marekani mgogoro mkubwa zaidi kuliko ule wa miaka 12 iliyopita. Ili kuzuia mgogoro wa kiuchumi unaotokana na corona; Rais Donald Trump wa nchi hiyo amesaini idhinisho la kiasi cha dola trilioni 2.2. Kwa mujibu wa idhinisho hilo, mamia ya mabilioni ya dola fedha taslimu zitagawiwa kwa raia wa Marekani, wafanyakazi, wamiliki wa shughuli ndogondogo na hatimaye mashirika makubwa yaliyoathirika na corona. 

Rais Donald Trump asaini kutolewa dola trilioni 2.2 kukabiliana na  athari za corona 

Wakati huo huo licha ya hatua hizo na ahadi zilizotolewa na viongozi wa Ulaya na Marekani lakini wasiwasi walionao wataalamu na wakuu wa masoko ya  fedha umepelekea kwa mara nyingine tena hali ya masoko ya fedha na hisa kukabiliwa na wakati mgumu na hivyo kutotilia maanani mikakati ya aina hii tajwa ya utoaji misaada ambayo nchi na benki kuu inaitekeleza ili kukabiliana na taathira za kuenea virusi vya corona kwa uchumi wa ulimwenguni. Kwa kadiri kwamba soko la hisa la Paris limethibitika kupuungua mwishoni mwa miamala yake siku ya Ijumaa ikilinganishwa na mwishoni mwa miamala ya kabla yake.   

Jeff Chapman Mkurugenzi wa Mradi wa Afya ya Taifa katika Taasisi ya PEW anasema: Majimbo yana machaguo machache sana na yanapasa kuwa na bajeti zenye mlingano pale mapato yanapoporomoka ghafla kama yanavyofanya hivi sasa. Yanalazimika imma kuongeza ushuru au kupunguza matumizi; machaguo ambayo yote mawili yanadhuru uchumi. 

James Bullard Mkuu wa Mfuko wa Shirikisho wa Saint Louis pia ameeleza kuwa: Kuna uwezekano kiwango cha ukosefu wa ajira katika miezi ijayo kikafika asilimia 30.   

Hali ya mambo katika nchi zinazoendelea ni mbaya zaidi. Ripoti za kimataifa zinaonyesha kuwa masoko ya nchi hizo yatahitaji karibu dola trilioni 2.5. Nao Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umetangaza kuwa hadi sasa nchi 80 zimewasilisha maombi kwa mfuko huo ya kupatiwa misaada ya fedha.  

Kuenea virusi vya corona na mamilioni ya watu kuwekwa chini ya karantini katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita kumeufanya uchumi wa dunia kukabiliwa na mgogoro mkubwa. Hata hivyo licha ya hatua zote zilizotekelezwa hadi sasa wachumi duniani wanataraji kushuhudia kuporomoka pakubwa hali ya uchumi katika historia ya  ulimwengu na hata kupindukia zaidi. Kwa msingi huo  hatua zilizochukuliwa sasa hazionekani kuwa zitasaidia kuepusha hali hii ya uchumi yenye kutia wasiwasi bali ni njia tu ya kuweza kutuliza mambo na kuvuka kipindi hiki kigumu. 

Tags