Wakazi wa New York walalamikia utendaji kazi mbaya wa WHO
(last modified Tue, 21 Apr 2020 11:14:57 GMT )
Apr 21, 2020 11:14 UTC
  • Wakazi wa New York walalamikia utendaji kazi mbaya wa WHO

Wakazi wa mji wa New York nchini Marekani wamelalamikia utendaji kazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu namna lilivyoamiliana na suala zima la kuenea virusi vya Corona.

Wakazi wa New York ambao ni moja ya miji ya mwanzoni ya Marekani kuathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi vya Corona, wametoa malalamiko yao dhidi ya shirika hilo kwa kile walichosema ni uzembe katika radiamali yake kufuatia maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19. Katika malalamiko yao, wakazi wa New York wamelikosoa Shirika la Afya Duniani kwa kutotangaza kwa wakati maambukizi ya Corona, kutokuwepo uangalizi juu ya maambukizi ya mwanzo ya virusi hivyo nchini China, kutotangaza kwa wakati miongozo ya tiba na kushirikiana na serikali ya China katika kuficha baadhi ya mambo kuhusu virusi hivyo.

Trump, mchochezi mkuu dhidi ya shirika la WHO

Hadi sasa Shirika la Afya Duniani (WHO) halijaonyesha radiamali yake kuhusu tuhuma hizo. Tuhuma hizo zimetolewa katika hali ambayo, ukosoaji juu ya utendaji kazi dhaifu wa serikali ya Washington katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini Marekani, umeshika kasi. Wiki iliyopita pia, Rais Donald Trump wa Marekani alitoa vitisho dhidi ya shirika hilo sambamba na kutangaza kukata msaada wa kifedha wa nchi yake kwa WHO. Katika kuhalalisha hatua yake hiyo, Trump alidai kuwa shirika hilo limeshindwa kutekeleza wadhifa wake juu ya kuenea virusi vya Corona na kwamba ni lazima lijibu tuhuma zinazolikabili. Aidha rais huyo wa Marekani alilituhumu shirika hilo la WHO kuwa linaipendelea China.

Tags