Ufaransa yamshambulia na kumtia mbaroni kiongozi wa taasisi ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64049-ufaransa_yamshambulia_na_kumtia_mbaroni_kiongozi_wa_taasisi_ya_kiislamu
Polisi ya Ufaransa imevamia nyumba ya kiongozi wa asasi moja isiyo ya kiserikali ya Waislamu wa nchi hiyo na kumtia mbaroni, katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu wa nchi hiyo ya Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 16, 2020 04:17 UTC
  • Ufaransa yamshambulia na kumtia mbaroni kiongozi wa taasisi ya Kiislamu

Polisi ya Ufaransa imevamia nyumba ya kiongozi wa asasi moja isiyo ya kiserikali ya Waislamu wa nchi hiyo na kumtia mbaroni, katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu wa nchi hiyo ya Ulaya.

Taarifa ya asasi hiyo inayoitwa BarakaCity imesema rais na muasisi wa shirika hilo lisilo la serikali, Idriss Sihamedi ametiwa mbaroni baada ya makazi yake kuvamiwa. Imesema maafisa wa polisi wa Ufaransa walimpiga na kumjeruhi vibaya Sihamedi kabla ya kumtia mbaroni.

Habari zaidi zinasema kuwa, wakati wa uvamizi huo, mkewe Sihamedi hakuruhusiwa kuvaa vazi la staha la hijabu, huku akitiwa pingu kwa nguvu na maafisa usalama wa Ufaransa.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Gerald Darmanin alidai katika ujumbe wa Twitter ambao baadaye aliufuta kuwa, Sihamedi anaunga mkono ugaidi kwa hali na mali, katika hali ambayo asasi anayoisimamia ya BarakaCity inatambulika kwa kuwafikishia misaada ya kibinadamu Waislamu wanaosumbuliwa na uchochole katika nchi za Togo, Palestina, Congo DR, Niger, na Syria.

Maandamano ya kupinga chuk dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa

Haya yanajiri chini ya masaa 48 baada ya serikali ya Ufaransa kuamua kufunga baadhi ya misikiti nchini humo ikiwa ni katika hatua zake dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu na Waislamu.

Viongozi wa serikali ya Ufaransa katika miezi ya karibuni wameshadidisha siasa na hatua zao za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Siku kadhaa zilizopita Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo pia alitoa hotuba dhidi ya Uislamu aliposema kwamba Uislamu upo katika mgogoro ulimwenguni kote. Katika mwendelezo wa sera za kupiga vita Uislamu nchini Ufaransa, Macron mwezi uliopita alizindua mpango wa kulinda thamani za kisekulari za nchi hiyo dhidi ya kile kilichotajwa kuwa "misimamo mikali ya Kiislamu."