Askari wa jeshi la majini la Uingereza ajiunga na Daesh
Imearifiwa kuwa askari mmoja wa jeshi la majini la Uingereza ameondoka nchini na kuelekea Syria kujiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Habari zinasema kuwa, Ali Alosaimi mwenye umri wa miaka 28 alipokea mafunzo ya hali ya juu ya ubaharia nchini Uingereza kwa miaka mitatu kabla ya kuondoka nchini na kwenda kujiunga na Daesh.
Gazeti la The Mail jana Jumapili lilichapisha habari za askari huyo wa baharini wa Uingereza mwenye asili ya Kuwait baada ya kupatikana nyaraka kumhusu katika shehena iliyokuwa na nyaraka za wanachama wa kundi hilo la kigaidi.
Admeri Lord West, mkuu wa zamani wa jeshi la majini la Uingereza amesema ana wasi wasi kuwa huenda kundi la Daesh linataka kuanzisha mbinu mpya ya hujuma zake. Amesema yumkini kundi hilo sasa linataka kuanzisha ugaidi wa baharini kwa kushambulia meli na feri, ndipo sasa limeanzisha kampeni za kuwashawishi askari wa baharini wa Uingereza wajiunge nalo.
Alosaimi anasemekana kupata mafunzo ya hali ya juu katika taaluma ya ubaharia na jeshi la majini katika Chuo cha South Tyneside eneo la Tyne nchini Uingereza kati ya mwaka 2011 na 2013.