Feb 14, 2023 02:26 UTC
  • Indhari ya kuenea tishio la Daesh pasi na kutajwa waungaji mkono wake

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya katika ripoti yake ya kiduru kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, licha ya hasara na pigo kubwa lililopita kundi la kigaidi la Daesh katika miaka ya hivi karibuni lakini tishio la la kundi hilo la kigaidi lingali linaongezeka kwa ulimwengu.

Guterres amesisitiza katika ripoti yake hiyo kwamba, kundi la kigaidi la Daesh limo katika hali ya kupanua wigo wa harakati na upenyaji wake barani Afrika na ili kufikia lengo hilo, linatumia nyenzo na suhula za kisasa na hata droni.

Weixiong Chen, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Kupambana na Ugaidi Katika Umoja wa Mataifa anasema:  Daesh imo katika kukusanya nguvu na uwezo wake na kueneza satua na ushawishi wake katika maeneo mbali mbali barani Afrika.

Indhari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuchukua wigo mpana wa hatari na tishio la kundi la kigaidi la Daesh ulimwenguni hususan barani Afrika Afrika lnachukua maana hasa kwa kuzingatia matukio ya miaka ya hivi karibuni katika uga wa harakati za kundi la kigaidi la Daesh.

Marekani ikishirikiana na washirika wake katika eneo la Asia Magharibi imekuwa na mchango usio na kifani katika kuundwa na kupata nguvu kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kwa minajili ya kukabiliana na mhimili wa muqawama. Kadhalika Marekani ilikuwa na nafasi muhimu ya kuibuka na kupata nguvu kundi la Daesh huko Iraq, Syria na kisha nchini Afghanistan. Kuna ushahidi na nyaraka zenye nguvu na mashiko katika uwanja huu ambapo zinaonyesha jinsi serikali ya Washington ilivyochukua hatua na kuandaa mipango na mikakati katika uwanja huu.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani haiwezi kuficha na kukana nafasi na mchango wake muhimu wa kuundwa na kupata nguvu kundi la kigaidi la Daesh. Awali kundi la Daesh liliundwa huko Iraq kwa ushirikki wa mabaki ya wanachama wa chama cha Baath, masalafi na matakfiri waliokusanywa huko Iraq kutoka mataifa mbalimbali ya dunia na kwa harakati sana wigo wa harakati zake ukapanuka kutoka Iraq hadi nchini Syria.

Marekani ikiwa kinara wa madola ya Magharibi na ikishirikiana na waitifaki wake wa Kimagharibi na Kiarabu ilichukua hatua ya kuyasaidia kwa hali na mali makundi ya kigaidi na kitakfiri likiwemo la Daesh

Lengo la Marekani na washirika wake lilikuwa ni kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria chini ya uongozi wa Rais Bashar al-Assad na wakati huo huo kudhoofisha mhimili wa muqawama. Kimsingi, Marekani ililitumia kundi hilo na makundi mengine ya kigaidi kwa ajili ya kufikia malengo yake.

Donald Trump aliyekuwa Rais wa Marekani alitangaza katika hotuab yake kuhusu mchango wa moja kwa moja wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Barack Obama na Hillary Clinton aliyekuwa waziri wake wa mashauri ya kigeni katika kuanzishwa na kuundwa kundi la kigaidi la Daesh.

Akihutubia Januari 2016 katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, Trump alisema: Obama na Clinton sio watu wakweli. Wao ndio walioanzisha kundi la Daesh. Obama pamoja na Clinton walianzisha kundi la Daesh, alisisitiza.

Donald Trump

 

Matamshi ya Trump kimsingi yaliunga mkono na kuthibitisha tuhuma alizokuwa akikabiliwa nazo Barack Obama kutoka kwa baadhi ya viongozi wa dunia kama Rais Vladmir Putin wa Russia kuhusiana na nafasi ya moja kwa moja ya ikulu ya Marekani White House katika kuanzishwa na kuibuka kundi la kigaidi la Daesh.

Nukta ya msingi ni kuwa, Iran ikiwa bega kwa bega na mataifa ya Syria na Iraq ilikuwa na nafasi isiyo na mithili katika kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh. Hili lilibainika wazi tarehe 21 Novemba 2017 wakati Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa Kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) alipomuandikia ujumbe Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kutangaza kusambaratishwa na kufikia mwisho umri wa kundi la kigaidi la Daesh. Baada ya tukio hilo muhimu yaani kushindwa na kupata pigo kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria na Iraq na kuangamizwa serikali iliyojitangaza ya Daesh kulishuhudiwa wanachama wengi wa kundi hilo wakihamia katika maeneo mengine hususan kaskazini mwa Afrika. Ni baada ya hapo ndipo kulipoanza kushuhudiwa kwa ukubwa zaidi tishio la kundi la Daesh katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh

 

Nukta muhimu ni hii kwamba, Marekani na washirika wake ambao kimsingi wana historia kongwe ya kuliunga mkono na kulisaidia kila upande kundi la kigaidi la Daesh Agosti 2014 waliunda kile kilichojulikana kama muungano eti wa kupambana na Daesh. Kwa hatua yao hiyo, madola hayo yalitaka kujitoa kimasomaso na kuonyesha kwamba, yapo mstari wa mbele katika kupambana na Daesh. Hii ni katika hali ambayo, uongo na unafiki wa Marekani kuhusiana na hili uko wazi na bayana kabisa. Mwaka 2011 hadi 2014 Marekani ilikuwa ikilisaidia kwa kila namna kundi la kigaidi la Daesh na kuwa na nafasi muhimu katika kulipatia fedha na vifaa vya kilojistikki ambapo kama siyo misaada hiyo ya Washington, kundi la Daesh lisingeweza kutenda jinai zote zile za kutisha na kutia simanzi.

Linalosikitisha zaidi ni kwamba, licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutahadharisha kuhusiana na kupanuka tishio la kundi la Daesh barani Afrika hakuashiria hata kwa mbali waanzilishi wa kundi hilo au hata ambao kipindi fulani walilisaidia na kuliimarisha kwa namna moja au nyingine. Hii nayo yenyewe inaonyesha ni kwa namna gani, Umoja wa Mataifa nao haufanyi kazi zake kwa kujitegemea bali ni mwanasesere anayetumiwa na madola makubwa kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Tags