Mar 05, 2023 08:42 UTC
  • Sisitizo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela kuhusu uhusiano wa jadi na Iran

Ivan Khel Pinto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Al Mayadeen kwamba, uhusiano mzuri wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa muda mrefu, ni wa jadi na ni mkubwa.

Waziri Pinto pia amesema, ushirikiano wa karibu baina ya Caracas na Tehran unatokana na kwamba Iran ni muitifaki wa jadi wa Venezuela. Ameongeza kuwa, nchi yake imependekeza kuweko muungano wa kimkakati kati ya Tehran na Caracas kwa muda wa miaka 20 ijayo.

Katika mahojiano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ametoa tathmini kuhusu uhusiano wa nchi yake na Russia na Iran na kusisitiza kuwa, Caracas ina uhusiano wa karibu na Moscow na Tehran. Amesema, kuna miradi mingi inaendelea hivi sasa baina ya pande mbili katika nyuga za nishati, chakula, teknolojia ya mawasiliano pamoja na usafiri na uchukuzi. Ivan Khel Pinto, ameongeza kuwa, Rusia na Iran ni waitifaki wa jadi wa Venezuela akiongeza kuwa, Caracas muda wote inawasiliana na Tehran na Moscow na ina uhusiano madhubuti na miji mikuu hiyo miwili. Hata hivi karibuni kabisa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Venezuela walionana na kufanya mazungumzo ya kirafiki pambizoni mwa kikao ha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Bendera za Iran na Venezuela

 

Sisitizo la kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Venezuela kuhusu uhusiano wa jadi wa nchi yake na Iran umezingatia msimamo wa pande mbili wa kushirikiana kwa kuzingatia maslahi yao licha ya kutengana kwa masafa makubwa ya kijiografia. Iran iko Asia Magharibi, wakati Venezuela iko Amerika ya Latini, lakini hilo halijazuia nia njema ya mataifa haya mawili kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana kwenye nyuga tofauti. Lakini kama ilivyotarajiwa, katika miongo kadhaa ya hivi karibuni, uhusiano wa nchi hizi mbili umezihamakisha mno nchi za kibeberu hasa Marekani na muda wote inafanya njama dhidi ya nchi hizo. Hasa kwa kuzingatia kuwa, Iran na Venezuela pamoja na Chuba, Nicaragua na Bolivia, kwa muda mrefu zinapambana na siasa za kibeberu za madola ya Magharibi hususan Marekani.

Sayyid Muhammad Hosseini, Makamu wa Rais wa Iran anasema: Jamhuri ya Kiislamu ina uhusiano mzuri na nchi za Cuba, Nicaragua, Brazil, Chile, Venezuela na nchi nyingine za Amerika ya Latini na ni matumaini yetu serikalli mpya itaendeleza uhusiano huo katika nyuga tofauti.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Venezuela

 

Kiujumla ni kwamba Jamhuri ya Kiislalmu ya Iran imeamua kufuata siasa za kuisaidia Venezuela katika kukabiliana na mashinikizo ya Washington. Hatua ya Iran ya kuipelekea meli za mafuta Venezuela tena mara kadhaa baada ya kuwekewa mashinikizo makubwa na Marekani, ni sehemu ya utekelezaji wa siasa hizo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuisaidia Venezuela kukabiliana na mashinikizo ya Marekani.

Katika upande mwingine, inaonekana wazi kabisa kwamba siasa za Washington za uharibifu, kuzusha machafuko na kuendesha njama za mapinduzi dhidi ya Iran na Venezuela zimefeli vibaya sana na dola la kibeberu la Marekani limezidi kufedheheka. Hii ni katika hali ambayo, hatua ya karibuni kabisa ya kuimarishwa ushirikiano baina ya Iran na Venezuela ni kuanzishwa safari za moja kwa moja za meli baina ya nchi hizi mbili ndugu.

Katika taarifa yake, ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Caracas umetangaza kuwa, safari za moja kwa moja za meli baina ya Iran na Venezuela zilianza mwezi uliopita wa Bahman 1401 Hijria Shamsia kwa shabaha ya kutia nguvu biashara baina ya nchi mbili. Hatua hiyo inaonesh kuwa, licha ya kuweko mashinikizo na njama za kila namna za Marekani, lakini uhusiano wa Venezuela na Iran unazidi kuimarika, siku baada ya siku.

Tags