Netanyahu akaribishwa UK kwa maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina
Mamia ya waungaji mkono wa Palestina na wapinzani wa utawala haramu wa Israel wamefanya maandamano mjini London, kulaani safari ya Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu nchini Uingereza.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba bendera ya Palestina na mabango yenye jumbe za kuukashifu utawala wa Kizayuni wamekusanyika nje ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza katika barabara ya 10 Downing Street, kupinga safari ya Netanyahu nchini humo.
Kadhalika waandamanaji hao wameitaka serikali ya Uingereza kusitisha uungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Maandamano hayo yamefanyika huku Netanyahu akikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak chini ya ulinzi mkali.
Waandamanaji hao jijini London wamesikika wakipiga nara za kuunga mkono Intifadha ya Wapalestina, wakisisitiza kuwa mwamko na mapambano ndiyo njia pekee ya kuikomboa Palestina.
Mmoja wa waandamanaji hao ambaye anasema ni mwanachama wa Muungano wa Kuwatetea Wapalestina amenukuliwa akisema, "Serikali yetu inaunga mkono sera za Israel ikiwemo sera ya kijeshi, lakini tunawaambia Wapalestina kwamba sisi tunawaunga mkono."

Netanyahu alianza kukabiliwa na misukosuko hata kabla ya kusafiri kwenda Uingereza. Kwa mujibu wa gazeti la The Telegraph, mwanasiasa huyo mwenye misimamo mikali alilazimika kuakhirisha safari yake hiyo ya kuitembelea Uingereza, baada ya marubani kadhaa wa utawala huo kukataa kumsafirisha. Alitazamiwa kwenda nchi hiyo ya Ulaya tangu Alkhamisi ya juzi.
Netanyahu ameenda Uingereza huku maelfu ya walowezi wa Kizayuni wakiandamana kwa wiki 11 mfululizo sasa kupinga baraza la mawaziri wenye misimamo ya kufurutu ada la Netanyahu; na mpango wa mageuzi ya mahakama unaoshinikizwa na kiongozi huyo.