Trump ashtakiwa rasmi katika kesi ya utoaji "kiziba mdomo" kwa mwanamke muigizaji
(last modified Fri, 31 Mar 2023 07:10:22 GMT )
Mar 31, 2023 07:10 UTC
  • Trump ashtakiwa rasmi katika kesi ya utoaji

Mahakama kuu ya New York imemfungulia mashtaka rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ya kosa la kulipa pesa za kiziba mdomo kwa mwanamke muigizaji wa filamu za ngono kuelekea uchaguzi wa rais wa mwaka 2016.

Gazeti la New York Times, likinukuu vyanzo vya habari limeandika kuwa, baada ya uchunguzi uliofanywa na wakaguzi kwa siku kadhaa, baraza kuu la mahakama ya Manhattan limemshtaki rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, kwa kuhusika na kosa la jinai la kulipa kiziba mdomo.
Trump atakuwa rais wa kwanza wa Marekani kushtakiwa kwa kosa la jinai kwa kulipa kiziba mdomo cha dola 130,000 kwa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels.
Daniels, ambaye jina lake halisi ni Stephanie Clifford, alisema, alikuwa na uhusiano wa kingono na Trump, ambaye ameoa.
Aliyekuwa wakili wa Trump, Michael Cohen alithibitisha kuwa alimlipa muigizaji huyo fedha hizo kama kiziba mdomo kwa amri ya Trump.
Inasemekana kuwa mashtaka dhidi ya Trump yatatangazwa mnamo siku chache zijazo.
Habari ya kesi ya Trump ilivyopokelewa

Wakili binafsi wa rais huyo wa zamani wa Marekani amethibitisha kuwa amekabidhiwa rasmi waraka wa shtaka hilo dhidi ya Trump kutoka mahakama ya Manhattan.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, Trump, ambaye hapo awali alikana kufanya kosa lolote na kutoa kauli kali za kukosoa uchunguzi uliofanywa dhidi yake, anatarajiwa kujisalimisha kwa mamlaka za sheria wiki ijayo, 
Kulingana na wasaidizi wa Trump, rais huyo wa zamani wa Marekani kwa sasa yuko kwenye jumba lake la kifahari liitwalo Marae-Lago katika jimbo la Florida na kwamba ameshangazwa kusikia habari za kufunguliwa mashtaka ya kosa la jinai.
Timu ya wanasheria ya Trump imedai kuwa hakuna uhalifu wowote uliotendwa na kusisitiza kwamba baada ya rais huyo wa zamani wa Marekani kushtakiwa, ukweli utafichuka na haki itatendeka.
Familia ya Trump mwenyewe pia imekosoa vikali shtaka dhidi yake ikisema kwamba hiyo ni hatua ya "kumwandama kifursa mpinzani wa kisiasa katika mwaka wa kampeni za uchaguzi".
Baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani pia vimeripoti kuwa rais huyo wa zamani atakamatwa mnamo siku chache zijazo.../

 

Tags