Jun 06, 2021 07:55 UTC
  • Amisom kuchunguza kikamilifu madai kwamba KDF inaua raia wa Somalia

Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) umeahidi kuchunguza madai yanayosema kwamba, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limewaua raia katika eneo la Gedo nchini Somalia katika shambulizi la anga dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab.

Taarifa iliyotolewa jana jioni na AMISOM ilisema itafanya uchunguzi iwapo jeshi la Kenya,  KDF, ambalo ni sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM), lilikiuka kanuni za utendaji au la.

Taarifa hiyo imesema: AMISOM itachunguza kikamilifu tukio hilo na matokeo ya uchunguzi huo yatawasilishwa kwa pande zote husika."

Mapema Jumamosi, maafisa wa serikali ya Kenya walitaka maelezo kutoka kwa AMISOM, ambayo wamesema ndiyo inayesimamia itifaki yote ya utendaji wa wanajeshi wanaotumika chini ya mwavuli wa ujumbe huo wa Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Itakumbukwa kwamba, serikali ya Somalia kwa mara nyingine tena imekosoa vikali kile ilichodai kuwa ni tabia ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuua raia wa Kisomali katika mashambulizi yake ya anga katika eneo la Gedo, jimbo la Jubaland kusini mwa Somalia.

Wapiganajii wa al Shabaab, Somalia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imeashiria operesheni ya hivi karibuni ya KDF katika eneo la Gedo na kusisitiza kuwa, raia kadhaa wa Kisomali waliuawa katika hujuma za anga zilizofanywa na wanajeshi hao wa Kenya mnamo Juni 3.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema jeshi la Kenya lilifanya mashambulizi ya anga ya kiholela dhidi ya miji ya El-Adde na Hisa-u-gur kwa madai ya kuyalenga maficho ya wanamgambo wa al-Shabaab, lakini yaliishia kuua raia wasio na hatia.

Tags