Jan 05, 2021 11:47 UTC
  • Nukta nne muhimu katika hotuba ya Sayyid Nasrullah kwa mnasaba wa hauli ya Qassim Suleimani

Hotuba ya Samahat Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja tangu wauawe shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq maarufu kama Al-Hashd Al-Shaabi ilikuwa na nukta kadhaa muhimu na zenye mazingatio makubwa.

Moja ya nukta muhimu katika hotuba ya Sayyid Nasrullah ya hauli ya makamanda hao wa muqawama ni sisitizo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kuwaunga mkono waitifaki wake wa kieneo. Kimsingi ni kuwa, moja ya vigezo vya kimuamala vya madola yenye nguvu ni kuwa na waitifaki wa kieneo, waitifaki ambao wanalinda maslahi na usalama wa dola lenye kuwaunga mkono na kuwapatia himaya.

Hapana shaka kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dola lenye nguvu katika eneo la Asia Magharibi na nguvu hii athirifu imethibitisha kwamba, inazingatia maslahi na usalama wa waitifaki wake katika mazingira yoyote yale. Kwa maneno mengine ni kuwa, kuna uhusiano wa pande mbili baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watifaki wake wa kieneo.

Katika fremu hiyo, Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon akasema katika hotuba yake hiyo kwamba: Katika kipindi cha vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Lebanon, licha ya kukabiliwa na vita vya kulazimishwa dhidi yake na utawala wa diklteta Saddam, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuutupa mkono muqawama kama ambavyo katika vita vya Syria, Tehran ilitoa himaya na uungaji mkono wa dhati kwa serikali na wananchi wa nchi hiyo.

Mashahidi qassim Suleimani na Abu mahdi al-Muhandis

 

Nukta nyingine muhimu katika hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ilibainisha ukweli huu kwamba, kuuawa shahidi makamanda wa muqawama katu hakuwezi kusitisha harakati hiyo. Uhakika  na uhalisia wa mambo ni kuwa, kuuawa shahidi ni moja ya thamani muhimu katika mhimili wa muqawama. Makamnada wa muqawama katu hawana hofu na kifo, bali wanalikaribisha kwa mikono miwili na moyo mkunjufu kabisa suala la kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika dini ya Uislamu.

Taathira muhimu pia ya kuuawa shahidi ni kuelekea mhimili wa muqawama upande wa kuimarika na kupata nguvu zaidi. Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon sambamba na kubainisha kwamba, mhimili wa muqawama umefanikiwa kuvuka salama tukio la kuuawa shahidi makamanda wa muqawama amesisitiza kuwa: Mhimili wa muqawama kila unapopoteza kamanda wake, basi huwa na nguvu zaidi kama ambavyo huwa macho zaidi.

Matamshi haya ya Sayyid Nasrullah ni mfano na kigezo cha wazi cha mtazamo huu kwamba, shahidi Qassim Suleimani amekuwa hatari na tishio zaidi kwa maadui kuliko kabla ya kuuawa kwake shahidi. Huu ni ukweli ambao Marekani, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya mataifa ya Kiarabu yameshindwa kuudiriki; na ndio maana yanaendelea kufanya makosa ya kistratejia kama kuwaua makamanda wa muqawama.

Mashahidi Qassim Suleimani na Abu Mahdi al-Muhandis waliuawa 3.01.2020 kwa amri ya Rais Donald Trump katika shambulio la anga jirani na uwanja wa ndege wa Baghdad, Iraq

 

Kama alivyosema Samahat Sayyid Nasrullah ni kuwa, Wamarekani walikuwa wakidhani kwamba, kwa kumuua shahidi Hajj Qassim, wangefanikiwa kukata kiunganishi cha muqawama. Lakini hilo halijatokea. Moja ya taathira ya kuuawa shahidi Qassim Suleimani na Abu Mahdi al-Muhandis ni kuibuka nara na takwa la kutimuliwa wanajeshi wa Marekani katika eneo.

Katika hotuba yake hiyo kwa mnasaba wa hauli ya mwaka wa kwanza tangu kuuawa shahidi Qassim Suleimani na Abu Mahdi al-Muhandis, Sayyid Nasrullah amesema, kama si kuuawa shahidi makamanda hao, nara za kutimuliwa askari wa kigaidi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi isingebadilika na kuwa kaulimbiu ya wananchi wa eneo hili ambayo wanataka ifikie natija.

Nukta ya nne muhimu katika hotuba ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kwa namna fulani ilikuwa ni kuashiria kudhalilika pakubwa Marekani mbele ya muqawama. Marekani na washirika wake ambao wameshindwa kupata mafanikio katika kukabiliana ana kwa ana na muqawama na kugonga mwamba malengo yao, wamekimbilia kwenye njia na mchezo mchafu wa mauaji, vikwazo na kuandaa orodha bandia ya ugaidi. Hata hivyo mauaji hayo yanazidi kuuimarisha muqawama kwa sababu, fikra ya muqawama na mapambano dhidi ya mataghuti chimbuko lake ni itikadi na mafundisho ya dini.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon akiwa na Luteni Jenerali Qassim Suleimani enzi za uhai wake

 

Vikwazo na kuandaa orodha bandia ya ugaidi ni mambo ambayo yameisukuma Marekani katika korongo la udhalili. Hii ni kwa sababu, madola makubwa duniani yamekataa kuungana na Marekani katika orodha hiyo ya ugaidi na hata orodha ya vikwazo nayo, haijaungwa mkono isipokuwa vinchi kadhaa vidogo ambavyo navyo vimelazimika kufanya hivyo kutokana na mashinikizo makubwa ya Washington. Kuhusiana na hili pia, Samahat Sayyid Nasrullah amesema: Marekani hivi sasa inazitaka nchi ambazo siyo mashuhuri na hata majina yake yanasikika kwa nadra sana zilitie jina la Hizbullah katika orodha yao ya ugaidi.

Nukta ya mwisho ni kwamba, makabiliano ya muqawama na Uistikbari wa Marekani na mapatano ya Waarabu na utawala bandia wa Israel, yameingia katika hatua na marhala mpya baada ya kuuawa shahidi makamanda shupavu wa muqawama wa Kiislamu Luteni Jenerali Qassim Suleimani na Abu Mahdi al-Muhandis. Hili ni jambo ambalo lilikuwa ajenda kuu katika hotuba ya Sayyid Nasrullah. Mauaji hayawezi kusimamisha muqawama, bali yanaongeza azma na irada zaidi ya kukabiliana na mabeberu.

Tags