Jun 08, 2021 02:47 UTC
  • Kambi ya muqawama haitaruhusu kuvunjiwa heshima al-Aqsa

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema wananchi wa Palestina na kambi ya muqawama katu hawataruhusu kuvunjiwa heshima Masjidul Aqsa.

Khadr Habib amesema hayo katika hotuba aliyoitoa jana Jumatatu ambapo alisisitiza kuwa, makundi ya muqawama yamesimama kidete na yako tayari kujibu mapgo kwa wanaopanga kuhujumu Msikiti wa al-Aqsa, katika mji wa Quds ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Habib amenukuliwa na shirika la habari la 'Falestin al-Yaum' akiwaonya Walowezi wa Kizayuni dhidi ya kufanya eti 'maandamano ya bendera' katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Ameeleza bayana kuwa, mrengo wa muqawama unafuatilia kwa karibu vitendo vya kihaini vya Wazayuni, na uko tayari kuchukua hatua yoyote inayohitajika kwa ajili ya kuihami Masjidul Aqsa.

Masjidul Aqsa

Kabla ya hapo, Yahya Sinwar, Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika Ukanda wa Ghaza ametoa tamko baada ya kubainika kuwa Wazayuni wanapanga kufanya shambulio jingine dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Yahya Sinwar kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Ghaza ameonya kuwa, iwapo Wazayuni watauhujumu tena msikiti wa al Aqsa basi harakati  za muqawama na mapambano zitauharibu mji wa Tel Aviv.

Tags