Jun 19, 2021 05:10 UTC
  • Wabunge Ufaransa wakosoa kuteuliwa afisa wa UAE kuongoza Interpol

Makumi ya Wabunge wa Ufaransa wamelalamikia hatua ya kuteuliwa afisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa Rais wa Polisi ya Kimataifa (Interpol).

Wabunge 35 wa Bunge la Taifa la Ufaransa wamemtaka Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo apinge uteuzi huo.

Katika barua yao, watunga sheria hao wameonya kuwa, Meja Jenerali Ahmed Naser al-Raisi anaelekea kuwa mkuu wa shirika la kimataifa la polisi lenye makao yake mjini Lyon katika hali ambayo, ana rekodi ndefu ya ukiukaji wa haki.

Wamesema Raisi anasimamia moja kwa moja jeshi la polisi la Imarati, ambalo lina faili jeusi la utendaji kazi, kwa kukiuka sheria na haki za binadamu.

Wabunge hao wa Ufaransa wamesema Meja Jenerali al-Raisi ni mhusika mkuu wa kamatakamata na kuzuiliwa kinyume cha sheria, mbali na kudhulumiwa na kuteswa watetezi wa haki za binadamu nchini humo.

Makao makuu ya Interpol

Mapema wiki hii, shirika huru la kutetea haki za binadamu la Persian Gulf Center for Human Rights (GCHR) lenye makao makuu yake mjini London liliwasilisha malalamiko katika mahakama moja ya Paris nchini Ufaransa, dhidi ya Raisi, Inspekta Jenerali katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Imarati.

Shirika hilo lilisema Raisi ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Kamati Kuu ya Interpol, ndiye anayebeba dhima ya mateso na kukadamizwa kwa Ahmed Mansoor, mwanaharakati mashuhuri wa demokrasia na mtetezi wa haki za binadamu wa Imarati, ambaye kwa sasa anazuiliwa katika gereza la kutisha la al-Sadr mjini Abu Dhabi.

Tags