Jul 07, 2021 02:21 UTC
  • Sisitizo la viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na China la udharura wa kuhuishwa JCPOA

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, na Rais Xi Jinping wa China wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kutoa wito kwa pande zinazofanya mazungumzo huko Vienna kwa ajili ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutumia vyema fursa iliyopo ya "Dirisha la Fursa" kwa ajili ya kufikia makubaliano kuhusiana na kadhia hiyo.

Viongozi hao aidha wamesisitiza juu ya ulazima wa kusukuma mbele gurudumu la mazungumzo kwa minajili ya kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo.

Sisitizo la viongozi wa nchi hizo tatu yaani China, Ujerumani na Ufaransa ambazo ni wanachama wa kundi la 4+1 juu ya udharura wa kutumiwa fursa iliyopo kwa ajili ya kulinda makubaliano ya nyuklia ya JCPOA lina umuhimu mkubwa hasa kwa kutilia maanani umuhimu wa makubaliano yenyewe kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa eneo na wa kimataifa.

Suala la kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA lina umuhimu maradufu hasa kwa madola ya Ulaya. Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya ambayo inaundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ikiwa inajumuisha wanachama kutoka Ulaya wa kundi la 4+1 mara kadhaa imedai kwamba, inataka kuhuishwa na kubakishwa makubaliano ya JCPOA hasa kwa kuzingatia umuhimu wa makubaliano hayo katika kulinda amani na usalama wa eneo na wa kimataifa. Madola hayo huko nyuma yaliahidi kwamba, yatafanya kile yawezalo kwa ajili ya kufikia lengo hilo.

China nayo kwa upande wake ikiwa mmoja wa wanachama wa mashariki wa kundi la 4+1 sambamba na Russia mataifa ambayo ni nguvu mbili kubwa za kimataifa zenye hitilafu za kimitazamo na Marekani nayo pia yana msimamo kama wa madola ya Ulaya katika uga huo. Kama alivyosema Rais Xin Jinping wa China ni kuwa, "JCPOA ni matokeo ya harakati ya pande kadhaa, na makubaliano haya yanapaswa kutekelezwa kwa namna yenye athari kutokana na umuhimu wake wa kuzuia wigo wa silaha za nyuklia na kuleta amani na uthabiti wa eneo la Asia Maghiribi.

 

Licha ya himaya na uungaji mkono wa wanachama wa magharibi na mashariki wa kundi la 4+1 wa kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini misimamo na utendaji wa Marekani katika uwanja huu ni jambo la kutia alama ya ulizo. Serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani inadai kwamba, kupitia mazungumzo ya sasa ya Vienna ambayo kwa njia isiyo ya moja kwa moja ina mawasiliano na Iran kupitia Kamisheni ya pamoja ya JCPOA inakusudia kuandaa mazingira ya lazima ya kurejea Marekani katika makubaliano hayo.

Serikali ya Rais aliyepita wa Marekani Donald Trump Mei mwaka 2018 alitangaza kuitoa rasmi Marekani katika makubaliano hayo. Kabla ya hapo na katika kipindi cha uongozi wake Trump alikosoa mara chungu nzima makubaliano ya JCPOA na kuyataja kuwa mabaya zaidi kwa Washington na akatishia kuitoa nchi yake katika makubaliano hayo.

Serikali ya Biden ambayo inadai kutaka kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kivitendo imechukua mkondo na utendaji ambao unaweza kupelekea kusambaratika makubaliano hayo. Katika mazungumzo ya Vienna, Marekani  imekariri matakwa yake ya kupenda makuu kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Iran vikiwemo "vipengee vya machweo".

Vipengee vya Machweo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA vinahusiana na kipindi cha kufikia tamati muda wa baadhi ya ahadi za Iran kwa mujibu wa makubaliano hayo. Katika upande mwingine, serikali ya Biden inataka kutiwa mambo mengine kama uwezo wa makombora wa Iran pamoja na siasa zake za kieneo katika makubaliano yoyote yale tarajiwa ambayo yatadhamini kurejea Marekani katika JCPOA na kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran vilivyowekwa katika kipindi cha Donald Trump.

Sambamba na hayo, serikali ya Biden imetangaza kuwa, haiko tayari kuondoa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran na kwamba, itaondoa vile vikwazo ambavyo inadhani kuviondoa kwake ni lazima kwa ajili ya kurejea katika makubaliano ya JCPOA.  Joseph Cirincione, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani anasema: Endapo Biden hatarekebisha mwenendo wake, kuna hatari ya kupoteza makubaliano muhimu ya nyuklia ya JCPOA.

 

Misimamo hiyo ya Marekani imeikasirisha pia Russia ambayo ni mmoja wa wanachama wa kundi la 4+1. Mikhail Ulyanov, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria aliashiria katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijami wa Twitter baadhi ya juhudi za kutaka kufuatilia masuala mapya ikiwemo kadhia ya usalama wa eneo na uwezo wa makombora wa Iran katika mazungumzo ya Vienna na kuandika: Hatua hizi ni mithili ya kufanya juhudi za kuua ndege kadhaa kwa jiwe moja, hatua ambayo haiakisi ukweli wa mambo na si ya kujenga. Lengo lililokubaliwa katika mazungumzo ya sasa ya Vienna ni kuhuisha tu makubaliano ya JCPOA.

Mikhail Ulyanov amebainisha kwamba, vipengee vya machweo sio sehemu ya mazungumzo ya kuhuisha JCPOA yanayoendelea huko Vinnea. Matamshi ya afisa huyo wa Russia yanaashiria juhudi za Marekanin ambayo inakusudia kutumia fursa ya mazungumzo ya Vieena kwa ajili ya kuishinikiza Iran na hivyo kupata upendeleo mkubwa. Hii ni katika hali ambayo, Tehran imetangaza kinagaubaga kwamba, imekuwa tayari kufanya mazungumzo kwa sura ya sasa na katu haitakubali hatua yoyote ya kutazama upya au kuongeza vipengee vyake vikiwemo vipengee vya machweo, kama ambavyo haiko tayari kufanya mazungumzo kuhusiana na maudhui ambazo kimsingi ziko nje ya makubaliano ya JCPOA ikiwemo kadhia ya uwezo wake wa makombora au siasa zake katika eneo.

Tags