Jul 22, 2021 02:27 UTC
  • Kirusi cha DELTA chapelekea hali ya corona Ufaransa kuwa mbaya sana

Waziri wa Afya wa Ufaransa amesema kuwa, hali ya maambukizi ya corona ni mbaya sana nchini humo kutokana na kuenea kirusi kipya cha DELTA ambacho kwa mara ya kwanza kiligunduliwa nchini India.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu waziri huyo wa afya wa Ufaransa, Olivier Véran akisema katika ripoti yake kuwa, idadi ya kila siku ya wagonjwa wa kirusi kipya cha corona kiitwacho DELTA imefikia hatua ya kuripuka na tayari wimbi la nne la maambukizo ya kirusi cha corona limeanza nchini Ufaransa. 

Amesema, idadi ya wagonjwa wa corona wa siku ya Jumanne kuamkia Jumatano na ambayo ilitangazwa jana ilionesha kuwa, katika kipindi cha masaa 24 zaidi ya watu 18,000 walikuwa wameambukizwa kirusi kipya cha corona kiitwacho DELTA huko Ufaransa. 

Waziri wa afya wa Ufaransa, Olivier Véran

 

Ufaransa ndiyo inayoongoza barani Ulaya kwa idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 (COVID-19). Hadi jana jioni, idadi ya Wafaransa waliotangazwa rasmi na serikali ya nchi hiyo kuwa wamekumbwa na ugonjwa huo ambao ni janga la dunia nzima walikuwa ni wagonjwa, 5,890,062. 

Ufaransa inafuatiwa na Uingereza kwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa UVIKO-19 barani Ulaya. Hadi jana jioni, serikali ya Uingereza ilikuwa imetangaza kuwa, imeshasajili wagonjwa 5,519,602 na vifo 128,823 vya wagonjwa wa corona, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi ya vifo vya ugonjwa huo barani Ulaya.

Marekani inaendelea kuongoza kwa mbali kwa idadi kubwa na wagonjwa na vifo vinavyotokana na UVIKO-19 duniani. Hadi jana jioni, Marekani ilikuwa imetangaza kusajili wagonjwa 35,082,093 na vifo vya wagonjwa 625,401 wa corona. Baada ya Marekani ni India, Brazil na Russia juu ya Ufaransa.

Tags