May 23, 2024 07:19 UTC
  • TZ yaitoa hofu UNHCR: Hatutafunga kambi wala kuwalazimisha wakimbizi warudi makwao

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema limepewa hakikisho na Serikali ya Tanzania kwamba kambi ya wakimbizi ya Nduta inayowapa hifadhi wakimbizi wa Burundi haitafungwa na wala wakimbizi hao hawatalazimishwa kurudi makwao.

Hakikisho hilo limetolewa na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania baada ya taarifa za habari zilizokuwa zimesambazwa hivi karibuni na vyombo vya habari vya nchi hiyo kueleza kwamba, wakimbizi wa Burundi wamefahamishwa na maafisa wa Tanzania kuhusu nia ya nchi hiyo ya kufunga kambi ya wakimbizi ya Nduta ambayo ni makazi ya zaidi ya wakimbizi 63,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu. 

Taarifa hizo zimedai kuwa huduma kwa wakimbizi zitasitishwa kutokana na kuzorota kwa hali ya maisha; na kwa hivyo wakimbizi wa Burundi watalazimika kurejea makwao, na kwamba hadhi ya ukimbizi itasitishwa kwa wakimbizi hao walioko nchini Tanzania.

UNHCR imesema, baada ya kupokea taarifa hizo ilikutana mara moja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania na kuzungumzia masuala hayo, na kusisitiza haja ya wakimbizi wote wanaorejea nchini mwao kuwa ni kwa hiari na kufuata Mkataba wa pande tatu wa kurejea kwa hiari kwa wakimbizi uliosainiwa Burundi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Burundi na UNHCR.

Kufuatia mazungumzo hayo, shirika hilo la UN limesema,  Serikali ya Tanzania imetoa hakikisho kwamba kambi hiyo itaendelea kuwa wazi, na hakuna atakayelazimishwa kurejea nyumbani.

Kwa mujibu wa UNHCR, tangu lilipoanza zoezi la kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari Septemba 2017, zaidi ya wakimbizi 230,000 wamerejea nyumbani Burundi kutoka nchi jirani, wakiwemo zaidi ya 168,000 kutoka Tanzania.../

Tags