Nigeria na Morocco kujenga bomba la kusafirishia gesi
Serikali za Nigeria na Morocco zimesaini hati ya makubaliano ya kujenga bomba la kusafirishia gesi ambalo litaziunganisha nchi mbili hizo pamoja na nchi nyingine za Afrika na bara Ulaya.
Geoffrey Onyema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria amesema muafaka huo ulisainiwa katika safari ya hivi karibuni ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco mjini Abuja na kuongeza kuwa, mradi huo wa bomba la gesi utawajumuisha washika dau wote.
Hata hivyo waziri huyo hajabainisha siku ya kuanza kujengwa bomba hilo na kiwango cha fedha zitakazotumika. Hata hivyo amesisitiza kuwa, mradi huo utafungua soko lenye ushindani la bidhaa hiyo sio tu kwa nchi za eneo, bali hata katika nchi za bara Ulaya.
Kadhalika nchi mbili hizo zilikubaliana kuimarisha uhusiano wao katika nyuga za kiviwanda na uzalishaji pamoja na kilimo-biashara.
Sio vibaya kuashiria hapa kuwa, mafuta yanachangia asilimia 70 ya pato la taifa la Nigeria ambapo tangu mwezi Agosti mwaka huu uchumi wa nchi hiyo umezorota kutokana na mashambulio na hujuma dhidi ya mabomba ya kusafirishia mafuta hususan katika eneo la Niger Delta na kushuka kwa bei ya mafuta.