Reuters: Marekani na Ulaya 'zinaiba dhahabu Afrika' kupitia Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53070-reuters_marekani_na_ulaya_'zinaiba_dhahabu_afrika'_kupitia_imarati
Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Reuters umefichua kuwa, tani za dhahabu zenye thamani ya mabilioni ya dola zinasafirishwa kila mwaka kwa njia za magendo kutoka Afrika kuelekea Marekani na nchi za Ulaya, huku Umoja wa Falme za Kiarabu ukitajwa kuwa lango kuu la biashara hiyo haramu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2019 23:50 UTC
  • Reuters: Marekani na Ulaya 'zinaiba dhahabu Afrika' kupitia Imarati

Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Reuters umefichua kuwa, tani za dhahabu zenye thamani ya mabilioni ya dola zinasafirishwa kila mwaka kwa njia za magendo kutoka Afrika kuelekea Marekani na nchi za Ulaya, huku Umoja wa Falme za Kiarabu ukitajwa kuwa lango kuu la biashara hiyo haramu.

Uchunguzi huo umebaini kuwa, kiwango cha dhahabu kinachotoka katika nchi za Afrika huwa kinasafirishwa nje ya nchi hizo kwa njia za magendo bila nchi husika kustafidi ipasavyo au kupata kodi.

Data za Idara ya Forodha ya UAE zinaonesha kuwa, Imarati iliagiza tani 446 za dhahabu zenye thamani ya dola bilioni 15 mwaka 2016, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kuagizwa na nchi yoyote ile duniani.

Kwa mujibu wa Reuters, kiwango hicho ni kikubwa mno ikilinganishwa na tani 67 za madini hayo ya thamani zilizoagizwa na Imarati mwaka 2006, zilizokuwa na thamani ya dola bilioni 1.3.

Ripoti ya shirika la habari la Reuters imebainisha kuwa, kiwango hicho cha dhahabu kilichotoka Afrika na kusafirishwa Marekani na nchi za Ulaya kupitia Imarati ni kikubwa mno ikilinganishwa na kiwango kilichotajwa na nchi za Afrika zinazozalisha madini hayo.

Wachimba dhahabu Kongo DR

UAE ilidai kuwa ilinunua dhahabu kutoka nchi 46 za Afrika mwaka 2016, lakini nchi 25 miongoni mwa hizo hazina data kuhusu mauzo hayo. Mwaka 2015, China ndiyo ilikuwa mnunuzi mkubwa dhahabu duniani, lakini mwaka 2016 Imarati iliipiku na kuwa maugizaji mkubwa wa maliasili hiyo maradufu ya China.

Baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimekuwa zikilalamika kuhusu uchimbaji dhahabu kinyume cha sheria na magendo ya madini hayo ni Kongo DR, Uganda, Chad, Niger, Ghana, Tanzania, Zimbabwe, Malawi, Burkina Faso, Mali na Sudan.