UN: Yumkini Imarati imehusika katika mashambulizi ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53327-un_yumkini_imarati_imehusika_katika_mashambulizi_ya_libya
Jopo la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa linatathmini mashambulizi ya makombora dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, sanjari na kuchunguza uwezekano wa kutumika ndege zisizo na rubani 'drone' za Umoja wa Falme za Kiarabu katika hujuma hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 07, 2019 03:26 UTC
  • UN: Yumkini Imarati imehusika katika mashambulizi ya Libya

Jopo la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa linatathmini mashambulizi ya makombora dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, sanjari na kuchunguza uwezekano wa kutumika ndege zisizo na rubani 'drone' za Umoja wa Falme za Kiarabu katika hujuma hizo.

Shirika la habari la AFP limeripoti hayo leo Jumanne na kufafanua kuwa, "Ripoti ya siri iliyovuja ya Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa Baraza la Usalama la umoja huo imeeleza bayana kuwa, wataalamu hao wamefanya uchunguzi na kubaini kwamba, kombora la Blue Arrow la angani hadi ardhini na ambalo halijawahi kutumiwa tena Libya, limetumika katika mapigano ya Libya."

Kombora hilo lililotumiwa kushambulia ngome za Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa linamilikiwa na nchi tatu tu ambazo ni UAE, China na Kazakhstan.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, Saudi Arabia, Imarati na Misri zinaunga mkono mashambulizi ya kudhibiti Tripoli ya jenerali muasi Khalifa Haftar.

Jenerali Haftar amevitaka vikosi vyake kushadidisha hujuma mwezi huu wa Ramadhani

Khalifa Haftar kamanda wa 'Jeshi la Taifa la Libya', tarehe 4 Aprili alianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli na kupelekea kuanza vita vikubwa baina ya vikosi vyake na vile vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, na ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Watu karibu 400 wameuawa hadi sasa tangu kuanza kushambuliwa mji mkuu Tripoli na wengine 1650 wamejeruhiwa, mbali na zaidi ya 50 elfu kulazimika kuyahama makazi yao.