Makumi ya wahajiri wa Kiafrika waghariki katika pwani ya Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53406-makumi_ya_wahajiri_wa_kiafrika_waghariki_katika_pwani_ya_tunisia
Makumi ya wahajiri wamepoteza maisha katika ajali ya kuzama boti katika pwani ya Tunisia, wakitokea pwani ya Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2019 22:30 UTC
  • Makumi ya wahajiri wa Kiafrika waghariki katika pwani ya Tunisia

Makumi ya wahajiri wamepoteza maisha katika ajali ya kuzama boti katika pwani ya Tunisia, wakitokea pwani ya Libya.

Shirika la habari la Tunis Afrique Presse linaloendeshwa na serikali ya Tunis limeripoti habari hiyo na kubainisha kuwa, wahajiri 70 waliaga dunia katika ajali hiyo ya jana Ijumaa katika pwani ya Tunisia.

Hata hivyo Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM linasema idadi ya wahajiri walioghariki katika ajali hiyo ya jana Ijumaa katika bahari ya Mediterania baada ya boti yao ya plastiki kuzama ni watu 50.

Kwa mujibu wa IOM, watu 16 walinusurika katika ajali hiyo iliyotokea umbali wa kilomita 40 katika upwa wa Sfax, kusini mwa mji mkuu wa Tunisia, Tunis.

Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka jana pia, wahajiri 80 walikufa maji baada ya boti yao kuzama katika fukwe za Tunisia.

Wahajiri wa Kiafrika katika safari hatarishi za kuelekea Ulaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilitangaza kuwa zaidi ya wahajiri elfu mbili waliaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka uliopita wa 2018.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.