Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yafichua: Kikosi cha jeshi la Ufaransa kinamsaidia Haftar
(last modified Fri, 23 Aug 2019 02:31:31 GMT )
Aug 23, 2019 02:31 UTC
  • Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yafichua: Kikosi cha jeshi la Ufaransa kinamsaidia Haftar

Maafisa wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya wamefichua kuwa kundi moja la jeshi la Ufaransa linalomsaidia jenerali mstaafu Khalifa Haftar limewajengea wapiganaji wa kiongozi huyo muasi kituo cha kurushia ndege zisizo na rubani katika bandari ya mafuta ya al Sidr huko kaskazini mwa Libya.

Maafisa hao wamesema kuwa, kundi hilo la jeshi la Ufaransa linasimamia operesheni za ndege zisizo na rubani ambazo zimekuwa zikilenga kituo na kambi ya anga ya mji wa Misrata na maeneo muhimu ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya huko mashariki na kusini mwa mji huo.

Ripoti zinasema kuwa kundi hilo la askari wa Ufaransa linaishi katika eneo lenye ulinzi mkali sana katika bandari ya Ras Lanuf.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, kundi jingine la jeshi la Ufaransa limepelekwa katika mji wa Hun huko katikati mwa Libya na linasimamia chumba cha operesheni na mashambulizi yanayoendelea kusini mwa mji mkuu wa Libya Tripoli. Askari hao wa Ufaransa wanamsaidia jenerali muasi, Khalifa Haftar katika jitihada zake za kutaka kuuteka mji wa Tripoli tangu Aprili mwaka huu.

Vita vya ndani Libya vimesababisha vifo vya maelfu ya watu

Mchambuzi wa masuala ya siasa ya Libya As'ad al Sharta' amesema Ufaransa inafunga kabisa njia zote za kupatikana suluhisho la kisheria na kimataifa la mgogoro wa Libya na iwakingia kifua wahalifu na watenda jinai za kivita nchini humo kwa kutumia kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwezi uliopita wa Julai pia jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya liligundua makomboya dhidi ya vifaru ya Ufaransa baada ya kuteka kambi iliyokuwa ikitumiwa na wapiganaji wa Jenerali Haftar.

Ufaransa, Misri na Imarati zinawasaidia wapiganaji wa Haftar kwa shabaha ya kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Tags