UN yazipongeza pande hasimu Libya kwa kuafikiana kufanyika uchaguzi
Umoja wa Mataifa umepongeza hatua ya pande hasimu za kisiasa nchini Libya kukubaliana kuitisha uchaguzi mkuu nchini humo katika kipindi cha miezi 18 ijayo.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya, Stephanie Williams amesema muafaka wa kuitisha uchaguzi umefikiwa katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika jana Jumatano huko Tunis, mji mkuu wa Tunisia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tunis ambako kunafanyika mkutano wa wajumbe 75 walioteuliwa na taasisi hiyo ya kimataifa kujadili mchakato wa amani wa Libya tokea Jumatatu, Williams amesema: Mkutano huu umefikia makubaliano ya awali, juu ya ramani ya njia ya kuelekea katika uchaguzi huru, wa haki, jumuishi na unaokubalika wa Bunge na Rais.
Mwanadiplomasia huyo wa Umoja wa mataifa ameongeza kuwa, pande hasimu katika mazungumzo hayo zimeafikiana juu ya kuziunganisha na kuzileta pamoja taasisi za nchi hiyo, kama sehemu ya mchakato wa amani ya kudumu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mousa Faki Mahammat alipongeza makubaliano ya kukomesha vita na mapigano nchini Libya yaliyosainiwa mjini Geneva, na kuyataja kuwa ni hatua muhimu katika njia ya kurejesha amani ya kudumu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Libya ilitumbukia katika lindi la vita na mapigano ya ndani mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi, na hivi sasa inatawaliwa na serikali mbili kinzani.