Zarif: Marekani wasifanye wachekwe, kamwe hawawezi kuipindua Jamhuri ya Kiislamu
(last modified Tue, 18 Jul 2017 07:43:08 GMT )
Jul 18, 2017 07:43 UTC
  • Zarif: Marekani wasifanye wachekwe, kamwe hawawezi kuipindua Jamhuri ya Kiislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya kijuba na yaliyo kinyume na misingi ya kimataifa yanayotolewa na viongozi wa Marekani wanaosema kuwa siasa zao kuu ni kufanya mapinduzi nchini Iran na kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu.

Viongozi wa Marekani akiwemo James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo wamekuwa wakisema hadharani kuwa wanaunga mkono njama za kuubadilisha utawala nchini Iran na eti uhusiano wa nchi mbili hauwezi kuwa nzuri hadi pale mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utakapopinduliwa. Dk Mohammad Javad Zarif, amelaani vikali ujuba wa viongozi hao wa Marekani na kusema kuwa, Wamarekani waangalie wasifanye watu wawacheke duniani kwani ni muhali kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ambayo nguvu zake ni uungaji mkono mkubwa wa wananchi. Amesema, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu una uhalali wa wananchi wa Iran kwani ni wao ndio waliopiga kura kutaka kutawaliwa na mfumo wa namna hiyo, hivyo njama zote za Marekani za kutaka kuupindua mfumo wa namna hiyo zitashindwa tu.

Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Amesema, tangu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Marekani haijawahi kuacha fursa yoyote ya kufanya njama za kuipindua Jamhuri ya Kiislamu  lakini imeshindwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, hivi karibuni wananchi wa Iran walishiriki katika uchaguzi wa rais wao; uchaguzi ambao uliongezewa muda mara kadhaa kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupiga kura, suala ambalo linaonesha ni kiasi gani wananchi wa Iran wanauunga mkono mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Vile vile amesema, hakuna nchi yoyote yenye demokrasia kubwa kama Iran katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Tags