Sep 16, 2022 07:40 UTC
  • Israel yamfuta kazi balozi wake anayetuhumiwa kuwabaka wanawake nchini Morocco

Utawala haramu wa Israel umelazimika kumfuta kazi balozi wake wa nchini Morocco anayekabiliwa na kashfa za ngono na kuwanyanyasa kijinsia wanawake wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala ghasibu wa Israel imetangaza kuwa, imemsimamisha kazi David Govrin balozi wake mjini Rabat na nafasi yake imechukuliwa na mwanamama Alona Fischer.

David Govrin aliyekuwa balozi wa Israel nchini Morocco hivi karibuni aligonga vichwa vya habari baada ya kuripotiwa ripoti kwamba, anakabiliwa na tuhuma kadhaa za kuwatumia vibaya wanawake, kuwabaka na kuwanyanyasa kijinsia.

Wiki iliyopita, mamia ya wananchi wa Morocco walifanya maandamano kulaani utovu wa kimaadili wa balozi wa utawala haramu wa Israel mjini Rabat baada vyombo vya habari kufichua kwamba, balozi huyo wa Israel mjini Rabat amehusika na udhalilishaji wa kingono wa wanawake wa nchi hiyo. Waandamanaji hao walichoma moto bendera za utawala haramu wa Israel na kutoa mwito wa kufungwa ubalozi wa Israel mjini Rabat.

Alona Fischer, balozi mpya wa Israel nchiini Morocco

 

Mwanadiplomasia huyo wa utawala dhalimu wa Israel ambaye tayari uchunguzi dhidi yake umeanza, anakabiliwa pia na tuhuma za ufisadi na kuiba zawadi ya thamani ya dola elfu 6 iliyotolewa na mfalme wa Morocco ambayo alipatiwa kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel lakini hakuikabidhi zawadi hiyo kwa Baraza la Mawaziri la Israel.

Kashfa za kimaadili zimeendelea kuhusishwa na wanadiplomasia wa Israel ambapo hivi karibuni mwanadiplomasia wa ubalozi wa Tel Aviv huko Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, alirejeshwa nyumbani kwa uchuunguzi kutokana na kukabiliwa na kashfa za kutenda uhalifu.

Tags