Ripoti: Israel inapanga kuwahamishia Afrika Wapalestina wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106822-ripoti_israel_inapanga_kuwahamishia_afrika_wapalestina_wa_gaza
Vyombo vya habari vya Israel vimethibitisha ripoti zinazodai kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya mazungumzo ya siri ili kuwahamisha kwa nguvu mamilioni ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na katika nchi nyingine za Afrika.
(last modified 2024-01-04T23:02:47+00:00 )
Jan 04, 2024 23:02 UTC
  • Ripoti: Israel inapanga kuwahamishia Afrika Wapalestina wa Gaza

Vyombo vya habari vya Israel vimethibitisha ripoti zinazodai kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya mazungumzo ya siri ili kuwahamisha kwa nguvu mamilioni ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na katika nchi nyingine za Afrika.

Tovuti ya habari ya Russia Today imenukuu ripoti ya gazeti la Times of Israel lililoandika kuwa, serikali ya Benjamin Netanyahu imefanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa Afrika ili kuwashawishi wakubali kuwapokea wakimbizi wa Kipalestina kutoka Gaza.

Gazeti hilo la Kizayuni limedai kuwa, DRC imeafikia pendekezo hilo la kuwapokea maelfu ya raia wa Palestina, na eti maafisa wa Tel Aviv wanafanya mazungumzo na viongozi wa mataifa mengine ya Afrika kwa ajili ya kuwapokea wakimbizi hao wa Kipalestina.

Jumapili iliyopita, Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich alitoa pendekezo la kutaka eti kupunguzwa idadi ya wakazi wa Gaza kwa milioni 2 na kubakisha laki 2 pekee, mpango ambao umeungwa mkono na unaendelea kupigiwa debe na maafisa wengine wa utawala huo pandikizi na waitifaki wake. 

Maandamano ya kupinga jinai za Israel huko Gaza

Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, unapinga kile kinachoonekana kama mpango wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, hatua haina tofauti na mauaji ya kimbari.

Aidha makundi ya muqawama ya Palestina yamelaani vikali mpango huo wa Israel wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu mamilioni ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kuwapeleka katika nchi nyingine na kusisitiza kuwa, pendekezo hilo limeweka bayana kuwa utawala huo haramu unaendeleza mauaji ya kimbari na jinai ya kivita katika eneo hilo la pwani lililozingirwa.