Uingereza inahusika na utesaji wapinzani Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i16372-uingereza_inahusika_na_utesaji_wapinzani_bahrain
Uingereza imetuhumiwa kuwa inahusika na utesaji wa wapinzani unaotekelezwa na utawala wa kiimla nchini Bahrain.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 30, 2016 07:33 UTC
  • Uingereza inahusika na utesaji wapinzani Bahrain

Uingereza imetuhumiwa kuwa inahusika na utesaji wa wapinzani unaotekelezwa na utawala wa kiimla nchini Bahrain.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadmau la Reprieve, limesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza inaendesha mpango maalumu wa kuwapa mafunzo askari wa utawala wa Bahrain, ambao wanahusika katika mateso ya kinyama na udhalilishaji wa wapinzani katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Ripoti hiyo imetoa wito kwa shirika la NI-CO linalohusika na kutoa mafunzo kwa askari wa Bahrain kusitisha mara moja mpango huo. Shirika hilo lilipata kandarasi ya Pauni 900,000 kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza kutoa mafunzo kwa askari wa Bahrain.

Shirika la Reprieve linasema wataalamu wa NI-CO wametoa mafunzo kwa askari magereza wapatao 400 katika Gereza la Jau ambalo linawashikilia wafungwa wanaosubiri kunyongwa.

Askari wa Bahrin wakimzingira mwandamanaji

Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa tangu mwezi Februari mwaka 2011. Wananchi wa Bahrain wanataka marekebisho ya kisiasa, uhuru, uadilifu, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Utawala wa Bahrain umewanyima wananchi wa nchi hiyo haki zao zote mbali na kutumia mkono wa chuma kuwakandamiza wapinzani. Idadi kubwa ya watu wameuawa na wengine kujeruhiwa katika maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Aal Khalifa.