Wapalestina waitaka Uingereza kuomba radhi kwa kutoa Azimio la Balfour
Taarifa ya mwisho iliyotolewa na mkutano wa Wapalestina wanaoishi barani Ulaya imeitaka Uingereza kuomba radhi rasmi kwa sababu ya kutoa Azimio la Balfour lililopelekea kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na hatimaye kufukuzwa wenyeji katika ardhi na nchi yao.
Mkutano huo ambao umefanyika Rotterdam nchini Uholanzi kukumbuka mwaka wa mia moja tangu kutolewe Azimio la Balfour, umesema kuwa azimio hilo lilikuwa makosa makubwa yasiyosameheka na kinyume na vigezo vya kibinadamu, uadilifu na haki za binadamu, na matokeo yake yalikuwa kughusubiwa haki za taifa la Palestina na nchi yao.
Taarifa ya mkutano huo imesisitiza kuwa, taifa la Palestina litaendelea kuwa na haki ya kukomboa nchi na ardhi yake licha ya kupita miaka mia moja sasa tangu kutolewe Azimio la Balfour. Taarifa ya wakimbizi wa Palestina barani Ulaya pia imetilia mkazo udharura wa kususiwa utawala ghasibu wa Israel, kuondoa vitega uchumi vya kigeni katika makampuni ya utawala huo dhalimu, haki ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika ardhi na nchi yao iliyotwaliwa na Wazayuni na tahadhari juu ya maafa ya kuendelea kuzingirwa eneo la Ukanda w Ghaza na taathira mbaya za kuhamisha balozi za nchi mbalimbali kutoka Tel Aviv kwenda katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem).
Azimio la Balfour lilitolewa mwaka 1917 na Waziri wa Mshauri ya Kigeni wa wakati huo wa Uingereza Arthur James Balfour akieleza uungaji mkono wa serikali ya London kwa mpango wa kuanzisha eti "nyumba ya kitaifa kwa ajili ya Wayahudi" katika ardhi ya Palestina. Azimio hilo ndilo lililokuwa msingi wa kuundwa dola haramu la Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.