Netanyahu aipongeza Imarati kwa kuialika Israel katika Maonyesho ya Dubai
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53110-netanyahu_aipongeza_imarati_kwa_kuialika_israel_katika_maonyesho_ya_dubai
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameupongeza Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuualika utawala huo haramu kushiriki katika Maonyesho ya Dubai ya 2020.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 26, 2019 22:10 UTC
  • Netanyahu aipongeza Imarati kwa kuialika Israel katika Maonyesho ya Dubai

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameupongeza Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuualika utawala huo haramu kushiriki katika Maonyesho ya Dubai ya 2020.

Katika taarifa, Benjamin Netanyahu amesema, "Tunawapongeza waandalizi wa maonyesho hayo kwa kuialika Israel, tunakaribisha kwa mikono miwili ushiriki wa Israel katika maonyesho hayo ya Dubai."

Netanyahu amesema kualikwa Israel katika maonyesho hayo ya kimataifa kunaonesha namna Tel Aviv inavyoendelea kutambuliwa kieneo na kimataifa.

Waandalizi wa maonyesho hayo ya kibiashara na ubunifu wamesema nchi 192 zimealikwa kushiriki maonyesho hayo, na kwamba utawala haramu wa Israel utashiriki pia.

Maonyesho hayo ya kibiashara ya Dubai Expo 2020 yanatazamiwa kufanyika kuanzia Oktoba 20 mwaka ujao hadi Aprili 20 mwaka 2021.

Mzayuni aliposhiriki mashindano ya Judo Imarati miezi michache iliyopita

Haya yanaripotiwa siku chache baada ya ujumbe wa kibiashara na kisiasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushiriki kwa siri kubwa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama nchini Bahrain kati ya Aprili 15 na 18, licha ya waandalizi wa mkutano huo kudai kuwa Wazayuni hao hawataushiriki kutokana na sababu za kiusalama.

Baadhi ya nchi za Kiarabu zimekuwa zikifanya juu chini kuboresha uhusiano na utawala khabithi wa Kizayuni unaoukalia kwa mabavu mji wa Quds, kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu duniani.