Watunisia waandamana dhidi ya Israel, waiunga mkono Palestina
Makumi ya wanaharakati wa kisiasa na kijamii wa nchini Tunisia kwa mara nyingine wamefanya maandamano katika barabara za mji mkuu Tunis, kulaani mpango wowote wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, sambamba na kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina.
Katika maandamano hayo ya jana Jumamosi, waandamanaji wamesikika wakipiga nara za kuulaani utawala haramu wa Israel na sera zake dhidi ya Wapalestina.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yenye maandishi ya kuilaani vikali Israel na kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Wananchi wa Tunisia katika maandamano hayo wamewataja viongozi wa nchi za Kiarabu kuwa 'wasaliti' huku wakitaja jitihada za kufanya wa kawaida uhusiano wa nchi hizo na utawala wa Kizayuni wa Israel kama uhaini.
Hali kadhalika wamesikika wakilaani vikali njama za Marekani dhidi ya Wapalestina, zilizopewa jina la 'Muamala wa Karne' wakisisitiza kuwa, mpango huo ni njama za Washington za kutambua na kuhalalisha sera za kibaguzi (apartheid) za Israel katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu.
Mwaka uliopita, Watunisia walifanya maandamano mengine kwa siku kadhaa mfufulizo wakilitaka bunge la nchi hiyo lifanye haraka kupitisha sheria ambayo itatamka wazi kuwa ni uhalifu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.