Marekani yaendelea kupora mafuta ya Syria, malori 30 yahamishiwa Iraq
(last modified Sun, 20 Sep 2020 07:47:30 GMT )
Sep 20, 2020 07:47 UTC
  • Marekani yaendelea kupora mafuta ya Syria, malori 30 yahamishiwa Iraq

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa, askari wa jeshi la kigaidi la Marekani wameiba malori 30 ya mafuta ya nchi hiyo na kuyahamishia nchi jirani ya Iraq.

SANA limetangaza kuwa, vikosi vya jeshi vamizi la Marekani, usiku wa kuamkia leo viliyaongoza malori hayo 30 ya mafuta yaliyoporwa katika eneo la Aljazira katika mikoa miwili ya Al Hasakah na Deir ez-Zur na kuyahamishia Iraq kupitia kivuko cha Al Walid.

Vikosi vya jeshi la kigaidi la Marekani, vikishirikiana na vikosi vya Wakurdi wa Syria vijulikanavyo kama Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria SDF ndivyo vinavyodhibiti akthari ya visima vya mafuta vya Syria katika eneo la Al Jazira.

Askari wa jeshi la kigaidi la Marekani wakiwa ndani ya ardhi ya Syria

Serikali ya Syria imeshasisitiza mara kadhaa kuwa vikosi vya jeshi la kigaidi la Marekani na vikosi vyenye mfungamano navyo vilivyoko huko mashariki na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo havina lengo jengine ghairi ya kupora mafuta ya nchi hiyo na vinapaswa kuondoka katika eneo hilo.

Jamii za makabila na kaumu mbalimbali za Syria zimekuwa zikifanya mikusanyiko na maandamano kwa muda mrefu sasa zikisisitiza kuwa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Marekani ndio unaohusika na kuchafuka kwa amani na wizi wa mafuta unaofanywa katika mikoa ya Deir ez-Zur na Al Hasakah na zimetaka vikosi hivyo vitimuliwe katika maeneo hayo.../

Tags