Hizbullah yapongeza juhudi za Iran za kusuluhisha matatizo ya eneo
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amepongeza sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na ugaidi sambamba na jitada zake za kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazolikabili eneo hili la Mashariki ya Kati.
Katika mazungumzo na Hussein Amir Abdullahian, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran anayesimamia maswala ya nchi za Kiarabu na Afrika huko mjini Beirut nchini Lebanon, Sayyid Nasrullah amesema: "Pande ambazo zinashinikiza malengo yao kupitia nguvu za kijeshi, ndizo zinazosababisha ukosefu wa usalama na kuenea kwa harakati za kigaidi katika eneo."
Kwa upande wake, Hussein Amir Abdullahian, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran anayesimamia maswala ya nchi za Kiarabu na Afrika ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kutokana na mauaji ya kamanda mwandamizi wa harakati hiyo, Mustafa Badruddin.
Badruddin mwenye umri wa miaka 55 na ambaye mbali na kuwa mkuu wa tawi la kijeshi la Harakati ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah na kukiongoza kikosi kinachoisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu, aliuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh mjini Damascus siku chache zilizopita.
Aidha, afisa huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo na familia ya shahidi Badruddin, ambaye pia alifahamika kama Dhulfiqar.