Nov 30, 2023 09:43 UTC
  • Wito wa Umoja wa Mataifa kuhusu usitishaji vita wa kudumu huko Gaza na onyo la kuenea mapigano

Siku ya Jumanne, ikiwa ni siku ya tano ya usitishaji vita wa muda huko Gaza, Umoja wa Mataifa ulifanya vikao viwili, kimoja katika Baraza Kuu kuhadili vita kati ya Israel na Hamas na kingine katika Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati na Syria, ambapo vikao vyote viwili vilizungumzia kuenea mapigano katika eneo na kusisitiza juu ya udhrura wa kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu.

Wawakilishi wa nchi mbalimbali katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa kuzingatia kuzorota hali ya kiafya na kimaisha ya watu wa Ukanda wa Gaza, walitoa wito wa kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu na kuandaliwa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya dhati kwa ajili ya kufikiwa suluhu ya kudumu na ya kiadilifu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia lilifanya kikao kuhusu Mashariki ya Kati na Syria, na kwa kutilia maanani vita kati ya Israel na Hamas, baadhi ya nchi zikatahadharisha kuhusu hatari ya kuenea migogoro katika eneo zima la Mashariki ya Kati na hasa nchini Syria.

Kufanyika vikao viwili hivyo katika Umoja wa Mataifa kunaonyesha wasi wasi wa jamii ya kimataifa kuhusu hali ya kulegalega na machafuko katika Ukanda wa Gaza na uwezekano wa kuenezwa vita na utawala haramu wa Israel katika nchi nyingine za Asia Magharibi hususan Syria. Baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, ambayo ilikuwa jibu la kuendelea vitendo vya ukatili na vya unyakuzi wa ardhi za Wapalestina vinavyofanywa na Tel Aviv, utawala wa Kizayuni ulitumia fursa hiyo kutekeleza jinai za kinyama na kivita dhidi ya raia wa kawaida wa Ukanda wa Gaza, na hasa watoto na wanawake wasio na hatia, ukidhani kuwa ungeweza kuwafutilia mbali kabisa wapiganahi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas na makundi mengine ya mapambano ya ukombozi wa Palestina katika ukanda huo.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Hata hivyo, matokeo ya mashambulizi ya nchi kavu ya utawala wa Kizayuni huko Gaza yamekuwa kinyume na utabiri wa viongozi watendajinai wa utawala huo, ambapo yameambatana na hasara kubwa ya vikosi na zana za utawala wa Kizayuni. Hivyo, kinyume na nara zao za awali zilizosisitiza kuendelea vita hadi kuangamizwa kabisa Hamas, viongozi hao wamelazimika kukubali usitishaji vita tena kwa masharti yaliyowekwa a Hamas yenyewe. Wamekubali usitisha vita wa siku 4 uliorefushwa kwa siku 2 na kisha siku nyingine moja. Jambo muhimu ni kwamba hapajakuwa na dhamana yoyote ya kuendelea usitishaji vita huo, na kumekuwepo na baadhi ya kesi ambapo Wazayuni wamekiuka mapatano ya usitishaji mapigano. Jambo hilo limezifanya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kuwepo usitishaji vita wa kudumu huko Gaza na kuepushwa mauaji ya Wapalestina wasio na hatia. Wakati huo huo jinai za kutisha zilizotekelezwa na utawala wa Kizayuni wakati wa vita huko Gaza zimezifanya baadhi ya nchi kutaka kushughulikiwa suala hilo kisheria katika mahakama za kimataifa.

Kuhusiana na hilo, Alia Ahmed Bin Seif At-Thani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa, ambaye pia ni mmoja wa wapatanishi wa makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Israel na Hamas pamoja na usitishaji mapigano wa muda huko Gaza, kwa mara nyingine tena ametoa wito wa kuundwa kamati ya kimataifa ya uchunguzi kuhusu jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. Amesema: 'Wapalestina wa Gaza wanaishi katika hali mbaya zaidi ya kibinaadamu kutokana na mashambulizi ya Israel ambayo yamepelekea kuuawa shahidi, kujeruhiwa na kutoweka zaidi ya watu 50,000. Hatua ya askari wa utawala wa Israel ya kuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa, ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na hatua ya kuumiza hisia za Waislamu.

Suala jingine ambalo lilizungumziwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni onyo kuhusu kupanuka wigo wa vita vya Gaza na kuzikumba nchi nyingine za eneo, jambo ambalo bila shaka linaweza kutokea wakati wowote kwa kuzingatia utambulisho wa kichokozi, kijinai na kibabe wa utawala wa Kizayuni. Katika kikao hicho mwakilishi wa Syria alilaani "mashine ya mauaji ya Israeli" ambayo "imetekeleza jinai za kutisha dhidi ya ubinadamu" na kusema: Israeli "inalisukuma" eneo zima katika mzozo mkubwa zaidi.

Alia Ahmed Bin Seif at-Thani

Kwa kutilia maanani kuendelea kuwepo vikosi vya kivamizi vya Marekani katika ardhi ya Syria na mashambulizi ya anga yanayofanywa mara kwa mara na jeshi la utawala wa Kizayuni katika maeneo tofauti ya Syria, hivi sasa kuna uwezekano wa kupanuka wigo wa vita hivyo katika nchi hiyo kuliko wakati mwingine wowote. Suala hilo limeitia wasiwasi mkubwa Russia, ikiwa moja ya madola ya kimataifa yanayoshindana na Magharibi katika eneo, ambayo bado ina uwepo wa kijeshi katika nchi hiyo kutokana na mwaliko rasmi iliyopata kutoka kwa serikali ya Damascus. Vassily Nebenzia, Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema: "Hali ya Syria ni nyeti sana kutokana na kushadidi mzozo kati ya Palestina na Israel. Nchi hii kama walivyo majirani zake kadhaa katika eneo hilo, inakaribia sana kuingia katika mzozo mkubwa katika eneo."

Tags