Dec 25, 2023 05:52 UTC
  • Kuvunjika muungano wa baharini wa Marekani kwa kujiondoa Ufaransa, Uhispania na Italia

Marekani imetangaza kuunda Muungano wa Baharini ikiwa ni katika jitihada zake za kuendelea kuutetea kwa hali na mali utawala ghasibu wa Israel katika hujuma yake ya kinyama dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kukabiliana na mashambulizi ya Yemen katika Bahari Nyekundu dhidi ya meli zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel huko Palestina.

Muungano huo hivi sasa uko katika hali ya kusambaratika kwa kujiondoa nchi kadhaa za Ulaya. Katika tukio muhimu la karibuni, Ufaransa, Uhispania na Italia zimetangaza rasmi kutoshiriki kwao katika muungano wa baharini unaoongozwa na Marekani katika Bahari Nyekundu unaojulikana kama "Walinzi wa Ustawi" na kuzuia manowari zao za kivita kuwa chini ya uongozi wa Marekani. Nchi hizo tatu za Ulaya zimesisitiza kuwa zitashiriki tu katika operesheni za ziada za majini zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa, NATO au Umoja wa Ulaya, na sio Marekani. Awali, Rais Joe Biden wa Marekani alionywa kwamba hakuna mtu atakayetoa umuhimu kwa operesheni yake hiyo ya baharini. Ni wazi kuwa kujiondoa nchi tatu za Ulaya za Ufaransa, Italia na Uhispania katika muungano huo wa Marekani, ni ishara ya kusambaratika muungano huo wa majini.

Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) hapo awali ilitangaza  kujiunga nchi 20 na muungano huo wa wanamaji, lakini haikuzitaja nchi zenyewe. Hata hivyo, Australia awali ilikataa ombi la Marekani la kutuma meli zake za kivita kwenye Bahari Nyekundu ili kujiunga na muungano wa wanamaji  wa nchi kadhaa kwa kisingizio cha kulinda usalama wa njia za meli baharini.

Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, jeshi la Yemen limelenga meli kadhaa za utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu na Mlango Bahari wa Bab al-Mandab ikiwa ni katika kuunga mkono muqawama wa wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza. Jeshi la Wanamaji la Yemen awali lilitahadharisha kwamba, litaendeleza operesheni zake za kijeshi dhidi ya meli na maslahi ya adui Mzayuni hadi pale atakapokomesha hujuma zake huko Gaza na dhidi ya taifa la Palestina. Utawala wa Kizayuni, ambao umeshindwa kudhamini usalama wa meli zake, umeitaka Marekani kuutatulia tatizo hilo. Lakini kuunda muungano mpya wa wanamaji kwa uongozi wa Marekani hakujafanikiwa. Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alisema Alhamisi usiku kwamba lengo la muungano huo wa wanamaji ni kuilinda Israel na si meli za kimataifa na kusisitiza kuwa nchi yake itajibu mashambulizi yoyote ya Marekani. 

Mashambulizi ya Yemen dhidi ya meli za kibiashara zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel au zinazohusiana na utawala huo wa Kizayuni, licha ya kuwa yameisababishia Israel hasara kubwa ya zaidi ya asilimia 90 ya biashara zake za nje zinazofungamana na bahari, vilevile yameongeza kwa kiasi kikubwa gharama za biashara ya baharini duniani hasa kwa nchi za Magharibi. Hususan ikizingatiwa kuwa, lango bahari la Bab al-Mandab ni njia ya maji kwenye Bahari Nyekundu ambayo hudhamini asilimia 30 ya biashara na kutumiwa na meli za mizigo ulimwenguni.

Harakati ya kishujaa ya askari wa Yemen

Operesheni ya kufana ya jeshi la Yemen katika kutetea na kuwalinda watu wa Gaza imesababisha makampuni makubwa ya meli kusafiri umbali wa ziada wa kilomita elfu 25 hadi masoko ya Asia kupitia Afrika Kusini. Jambo hilo limepelekea mashirika na serikali nyingi kuishinikiza Marekani iulazimishe utawala wa Kizayuni uondoe mzingiro wake wa kidhalimu dhidi ya Ukanda wa Gaza. Majid Saftaj, mtaalamu wa masuala ya Palestina na Asia Magharibi anasema: Baada ya Wazayuni kuvamia Ukanda wa Gaza, Ansarullah ya Yemen ilifunga lango hilo kama njia ya kutoa mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni na mwitifaki wake Marekani. Kwa hivyo, hatua hiyo imepelekea zaidi ya asilimia 50 ya mashirika ya meli kubadili njia za usafiri ua kusimamisha kabisa shughuli zao za kutuma mizigo Israel na suala hilo limewasababishia hasara kubwa Wazayuni.

Hivi sasa baada ya kujiondoa nchi tatu muhimu za Ulaya katika muungano wa wanamaji wa Marekani katika Bahari Nyekundu, itakuwa vigumu kufikiwa malengo ya muungano huo hususan ya kukabiliana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni na meli zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hii ni pamoja na kuwa muungano huo utagharimika pakubwa katika kufuatilia na kutungua ndege zisizo na rubani za Yemen ambapo moja ya ndege hizo inagharimu dola elfu 2 pekee ikilinganishwa na kombora la dola milioni 2 linalotumika kutungua ndege kama hiyo. Tovuti ya Paltico imeandika kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ina wasiwasi wa kuongezeka gharama ya kunasa na kutungua ndege zisizo na rubani pamoja na kuharibu makombora yanayorushwa na jeshi la Yemen. Politico, huku ikiashiria kuzuia mara 38 meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani makombora ya Yemen, imeandika kwamba: Kombora moja la dola milioni 2 hutumika kufuatilia na kuharibu ndege isiyo na rubani ya Yemeni yenye thamani ya dola 2,000.

Kutangaza kujiondoa nchi tatu wanachama wa NATO za Ulaya katika muungano wa jeshi la wanamaji la Marekani kunaonyesha kutoaminika Washington na washirika wake. Wakati huo huo suala hilo linaoonyesha upinzani wao dhidi ya siasa za Marekani za kuipendelea  Israel, uungaji mkono wake usio na mipaka kwa mashambulizi ya umwagaji damu huko Gaza na upinzani wake dhidi ya usitishaji vita katika ukanda huo, suala ambalo limepelekea Yemen kuanzisha mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu na hivyo kuzisababishia hasara kubwa nchi za Magharibi. Huku akiashiria suala la kutengwa Marekani na washirika wake, Barbara Bodin, mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani na Mkurugenzi  wa Taasisi ya Mafunzo ya Kidiplomasia katika Chuo Kikuu cha Georgetown  anasema, washirika wengi wa Marekani, wanaamini kuwa siasa zake za kuunga mkono Israel zinakinzana wazi na siasa za Wamagharibi za kuwa pamoja na Ukraine.

Tags