DCI: Mwaka 2023 ndio mwaka umbaya zaidi kwa watoto wa Kipalestina
Kundi la kimataifa linalofanya kazi katika uwanja wa kulinda watoto duniani limeutaja mwaka 2023 kuwa mwaka wa mauaji ya kimbari ya watoto wa Kipalestina huko Gaza.
Ni baada ya kuthibitika kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umeua watoto wasiopungua elfu kumi tangu tarehe 7 Oktoba 2023 katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Kwa mujibu wa Press TV, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watoto (DCI) limetangaza kuwa, maelfu ya watoto wa Kipalestina wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 7 Oktoba na kuongeza kuwa, idadi ya watoto wanaouawa na Israel itaongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel katika maeneo ya makazi ya watu huko Gaza, na bado hakuna idadi maalumu ya watoto waliofukiwa kwenye vifusi kutokana na mashambulizi ya mabomu ya utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa taarifa ya kundi hilo la kimataifa, mwaka 2023, watoto wasiopungua 121 wa Kipalestina waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wakati huo huo, Wizara ya Elimu ya Palestina imetangaza kuwa, idadi ya wanafunzi wa Kipalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni imeongezeka na kufikia zaidi ya 4,200.

Katika ripoti yake, wizara hiyo imetangaza kuwa tangu kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza baada ya Oktoba 7 mwaka jana, wanafunzi 84 wameuawa shahidi na wengine 100 wamejeruhiwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.