Wafungwa 15 wa Guantanamo wahamishiwa Imarati
Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imewahamisha wafungwa 15 wa jela ya kutisha ya Guantanamo na kuwapeleka katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ukiwa ni uhamisho mkubwa zaidi wa wafungwa hao kufanywa na utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani.
Habari zinasema kuwa, 12 miongoni mwa wafungwa hao ni raia wa Yemen na watatu ni raia wa Afghanistan. Taarifa ya Pentagon imeipongeza Imarati kwa kukubali kuwapokea wafungwa hao wa Guantanamo, ikiwa eti ni katika juhudi za Washington za kutaka kuifunga jela hiyo ya mateso iliyoko nchini Cuba.

Haya yanajiri miezi michache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kukosoa vikali mienendo mibaya ya Marekani dhidi ya wafungwa wa jela hiyo. Amnesty International ilisema kuwa, kuwanyima huduma za lazima za matibabu wafungwa wa Gitmo, kunadhihirisha ni kwa kiasi gani serikali ya Marekani isivyoheshimu mikataba ya kimataifa. Aidha Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kupiga Vita Utesaji huko nyuma iliilaani Marekani kwa kukataa kuchunguza vitendo vya utesaji na unyanyasaji washukiwa wa ugaidi katika jela ya Jeshi la Marekani ya Guantanamo Bay.
Mapema mwaka huu, Pentagon iliwahamishia Ghana wafungwa wawili raia wa Yemen ambao walikuwa wamezuiliwa kwa zaidi ya muongo mmoja katika jela ya mateso ya Guantanamo Bay nchini Cuba.

Itakumbukwa kuwa, Obama aliahidi kufunga Gitmo katika kampeni zake za kuwania urais mwaka wa 2008 akidai kuwa jela hiyo imeichafulia jina Marekani kote duniani, lakini hakutekeleza ahadi yake hiyo.