Hujuma dhidi ya Uislamu yashika kasi nchini Uingereza
Wimbi na hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu limeshika kasi zaidi na kulitia wasiwasi Baraza la Waislamu nchini Uingereza.
Taarifa iliyotolewa na Baraza la Waislamu nchini Uingereza imeeleza wasiwasi kuhusu kasi na kushadidi wimbi la hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo na kutoa wito kwa maafisa wa serikali ya London kukabiliana na wimbi hilo linaloshika kasi zaidi siku baada ya siku.
Taarifa hiyo pia imewataka viongozi wa vyama vikubwa nchini Uingereza kuvunja kimya chao mbele ya mashambulizi na juhuma zinazofanywa dhidi ya Waislamu.
Baraza la Waislamu nchini Uingereza pia limekosoa mienendo isiyofaa dhidi ya Waislamu nchini humo na kutangaza kuwa: Waislamu wanasumbuliwa na mienendo isiyo ya kibinadamu wala kimaadili na kwamba huko Scotland pia kumeshuhudiwa vitendo ya kuchorwa nara na alama za kibaguzi zinazohusiana na Vita vya Msalaba kwenye kuta za misikiti.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Uingereza, Haroon Khan pia amewataka wahariri wa magazeti ya nchi hiyo kujiepusha na ubaguzi na sera za kueneza chuki dhidi ya Waislamu.
Mwezi uliopita Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu yenye makao yake mjini London iliitisha mkutano uliowakutanisha pamoja wanaharakati wa haki za binadamu wa Marekani na Ulaya ambao waliikosoa serikali ya Uingereza kutokana na kuunga mkono uhalifu na jinai zinazofanywa dhidi ya Waislamu.
Vilevile gazeti la Guardian la Uingereza limeandika ripoti kwamba, makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali nchini humo yanafanya jitihada za kuanzisha vita vya kiutamaduni kwa shabaha ya kueneza chuki dhidi ya Waislamu nchini Uigereza.