Korea Kaskazini yamwandikia barua katibu mkuu mpya kushitakia vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23011-korea_kaskazini_yamwandikia_barua_katibu_mkuu_mpya_kushitakia_vikwazo
Serikali ya Korea Kaskazini imemwandikia barua António Guterres, Katibu Mkuu Mpya wa Umoja wa Mataifa ikilalamikia hatua ya kuongezwa vikwazo vya umoja huo dhidi yake.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Jan 07, 2017 15:48 UTC
  • António Guterres na bendera ya Korea Kaskazini
    António Guterres na bendera ya Korea Kaskazini

Serikali ya Korea Kaskazini imemwandikia barua António Guterres, Katibu Mkuu Mpya wa Umoja wa Mataifa ikilalamikia hatua ya kuongezwa vikwazo vya umoja huo dhidi yake.

Baada ya majaribio ya makombora ya balestiki yaliyofanywa na serikali ya Pyongyang mwezi Januari na Septemba mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha maazimio mawili mazito yanayojumuisha vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

António Guterres, Katibu Mkuu Mpya wa Umoja wa Mataifa 

Shirika la habari la Korea Kaskazini limetangaza kuwa, mwakilishi wa nchi hiyo amewasilisha barua ya malalamiko katika ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katika barua hiyo, serikali ya Pyongyang imelalamika ikisema, inakuwaje kila inapofanya majaribio ya silaha zake za nyuklia au makombora ya balestiki, umoja huo unafanya haraka kuiwekea  vikwazo, katika hali ya kuwa, Marekani na baadhi ya nchi nyingine zimeshafanya maelfu ya majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya namna hiyo bila kuwekewa vikwazo?

Sehemu ya nguvu za Korea Kaskazini

Kadhalika Korea Kaskazini imevitaja vikwazo hivyo dhidi yake kuwa ni dhidi ya ubinaadamu na ni dhidi ya ustaarabu wa mwanadamu kwani vimeyaweka hatarini maisha ya raia wake. Pyongyang pia imemsisitizia Katibu Mkuu huyo Mpya wa Umoja wa Mataifa kuwa, itaendelea na mipango yake ya silaha za nyuklia na makombora, na kwamba inafanya hivyo kutokana na siasa za kiuhasama na vitisho vya nyuklia vya Marekani.

Baadhi ya makombora hatari ya Korea Kaskazini yanayoitia tumbojoto Marekani

Katika salamu alizozitoa kwa mnasaba wa mwaka mpya wa 2017, Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini alisema, nchi yake iko katika hatua za mwisho za kulifanyia majaribio kombora la balestiki la kuvuuka mabara.