Rais Emmanuel Macron: Shirika la kijeshi la NATO limekufa ubongo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57132-rais_emmanuel_macron_shirika_la_kijeshi_la_nato_limekufa_ubongo
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa sambamba na kuonyesha wasi wasi wake kuhusiana na iwapo Marekani itaendeleza ahadi zake katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO amesema kuwa, shirika hilo limekumbwa na kifo cha ubongo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 08, 2019 08:18 UTC
  • Rais Emmanuel Macron: Shirika la kijeshi la NATO limekufa ubongo

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa sambamba na kuonyesha wasi wasi wake kuhusiana na iwapo Marekani itaendeleza ahadi zake katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO amesema kuwa, shirika hilo limekumbwa na kifo cha ubongo.

Rais Macron ameyasema hayo katika mahojiano na jarida la kila wiki la Economist na kubainisha kwamba nchi wanachama wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya haziwezi kuitegemea Marekani kwa ajili ya kujilinda. Ameikosoa serikali ya Washington kwa kutokuwa na mawasiliano na wanachama wengine wa shirika hilo katika kuchukuliwa maamuzi ya kistratijia. Bila ya kutaja jina, ameashiria msimamo wa Marekani kuhusiana na mashambulizi ya Uturuki huko kaskazini mwa Syria na kusema: "Tunashuhudia hatua za hujuma zisizo na uratibu za mmoja wa wanachama wa NATO (yaani Uturuki) kwenye eneo ambapo kunayaweka hatarini maslahi yetu."

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wakivutana kuhusu jambo na Trump

Inafaa kuashiria kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akizishinikiza nchi nyingine wanachama wa NATO kuzidisha bajeti yao ya kijeshi ndani ya muungano huo, suala ambalo limezidisha tofauti za ndani katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Hivi karibuni pia wanachama wa muungano huo wa kijeshi walikosoa mashambulizi ya Uturuki katika eneo la kaskazini mwa Syria. Nchi wanachama wa NATO zinaamini kwamba serikali ya Ankara ilichukua hatua hiyo kwa kupewa baraka na Marekani.